Storm FM
Storm FM
9 July 2026, 6:33 pm

Mradi huo unatarajiwa kukamilika hivi karibuni huku kukiwa na matumaini makubwa kwa wakazi wa wilaya hiyo juu ya mradi huo.
Na Mrisho Sadick:
Kukamilika kwa mradi huo itakuwa fursa kwa wakazi wa wilaya hiyo Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA wilayani Nyang’hwale mkoani Geita umefikia asilimia 86 ya utekelezaji huku Serikali Kuu ikiwa tayari imetoa zaidi ya shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.
Kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Geita imetembelea nakukagua maendeleo ya mradi huo unaojengwa katika kijiji cha Iseni Kata ya Kakora wilayani Nyang’hwale kwa gharama ya zaidi ya shilingi Bilioni 1.6.
Kaimu afisa udhibiti ubora wa shule wilaya ya Nyang’hwale Frank Maguhu akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya kamati ya siasa ya CCM amesema unatekelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa majengo tisa na awamu ya pili pia utahusisha majengo tisa nakwasasa uko asilimia 86 ya utekelezaji.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholous Kasendamila amesema kukamilika kwa chuo hicho kutachochea maendeleo ya kiuchumi na kuwajengea vijana ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira huku akiagiza mapungufu yote yaliyobainika yafanyiwe kazi kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Geita Martine Shigela amesema licha ya wilaya za Geita na Chato tayari kuwa na vyuo vya VETA, ujenzi unaoendelea katika wilaya za Nyang’hwale, Mbogwe na Bukombe unaonesha dhamira ya Serikali kusogeza huduma hiyo karibu na wananchi nakwamba miongoni mwa kozi zitakazotolewa katika vyuo hivyo ni za sekta ya madini,

Mbali na mradi wa VETA Nyang’hwale, Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Geita pia imekagua miradi mingine ya maendeleo katika sekta za afya, elimu na miundombinu ya barabara, na kueleza kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wake huku ikisisitiza usimamizi madhubuti ili miradi hiyo ikamilike kwa ubora na kuwanufaisha wananchi.