

11 November 2024, 12:44 pm
Chama Cha Mapinduzi CCM wilaya ya Mbogwe kimekamilisha ujenzi wa Ofisi 17 za kata wilayani humo nakwamba nguvu inahamia kwenye ngazi ya matawi.
Na Mrisho Sadick:
Zaidi ya milioni 600 zimetumika kujenga Ofisi za CCM katika Kata 17 za wilaya ya Mbogwe Mkoani Geita ikiwa ni mkakati wa Chama hicho kuweka mazingira rafiki ya kufanyia kazi ili kuwahudumia wanachama na wananchi kwa wakati.
Ujenzi wa Ofisi hizo za Kata 17 na Ofisi moja ya CCM wilaya ya Mbogwe umefadhiliwa na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Mkoa wa Geita Evarist Gervas, akiwa katika Kata ya Nanda kukabidhi Ofisi mpya ya CCM amesema niwajibu wa kila mwanachama kukijenga Chama nakwamba licha ya ujenzi wa Ofisi hizo ametoa viti 1,900 vyenye thamani ya zaidi ya milioni 26 katika Ofisi hizo.
Katibu wa CCM wilaya ya Mbogwe Josephat Chacha amesema ujenzi wa Ofisi hizo umekuwa chachu ya Chama hicho kufanya kazi kwa ufanisi kwani hapo awali walikuwa wakipata wakati mgumu kuwahudumia Wananchi huku Diwani wa Kata ya Nanda Jumamos Mathias akimpongeza MNEC Evaristi kwa hatua hiyo.
Katika hatua nyingine MNEC Evarist amewakumbusha wanachama wa CCM kuendelea kujipanga kikamilifu kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kuwahamasisha wananchi kuwapigia kura wagombea wa CCM kwakuwa uchaguzi huu hakuna utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa.