Storm FM
Storm FM
20 June 2026, 5:31 pm

Jumla ya watu 9 wamejeruhiwa na wengine kunusurika huku mtu mmoja akifariki dunia kutoka na ajali hiyo ambayo ilitokea katika kata ya Nyamigota iliyopo wilaya ya Geita.
Na: Ester Mabula
Mtu mmoja amefariki dunia na wengine 9 kujeruhiwa katika ajali ya mabasi mawili kugongana katika kata ya Nyamigota, mamlaka ya mji mdogo Katoro mkoani Geita.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Kenneth Mwakasitu amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo mnamo June 19, 2026 akisema ajali hiyo inatajwa kusababishwa na mwendokasi na uzembe wa madereva barabarani.
Mwakasitu ameyataja mabasi yaliyopata ajali kuwa ni ya Kampuni ya Najimnisa iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kuelekea Geita na Basi la Manyama iliyokuwa ikitokea Jijini Mwanza kuelekea Ngara.

Mganga Mfawidhi Kituo cha Afya Katoro Yohana Kitutu amethibitisha kupokea majeruhi 9 na mwili wa mwanaume mmoja aliyetajwa kuwa ni kondakta wa gari la Kampuni ya Najimnisa.
Kitutu amesema majeruhi 4 walihudumiwa katika Kituo cha Afya Katoro na wengine walipewa rufaa katika Hospitali ya Katoro kwa matibabu zaidi na wote wanaoendelea vizuri huku baadhi ya mashuhuda na manusura wa ajali hiyo wakielezea hali ilivyokuwa.
