Storm FM
Storm FM
6 September 2026, 8:47 pm

Mradi huo unatarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi laki saba katika vijiji 19 vya kata sita za Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na kata 13 za Manispaa ya Geita.
Na Mrisho Sadick:
Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amemtaka mkandarasi anayetekeleza Mradi wa Maji wa Miji 28 wilayani Geita kuanza majaribio ya mradi huo mwezi Oktoba na kuukamilisha ifikapo Disemba mwaka huu ili wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama.
Waziri Aweso ametoa agizo hilo leo Septemba 06, 2026 baada ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 124 ambao umefikia zaidi ya asilimia 80 ya utekelezaji.
Amesema ameridhishwa na kasi ya utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kunufaisha zaidi ya wananchi laki saba katika vijiji 19 vya kata sita za Halmashauri ya Wilaya ya Geita pamoja na kata 13 za Manispaa ya Geita.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mjini Geita (GEUWASA) Mhandisi Frank Changawa amesema mradi huo ukikamilika utaondoa changamoto ya maji kwa asilimia 100 huku miundombinu yake ikitarajiwa kutoa huduma kwa wananchi kwa kipindi cha miaka 20 mfululizo pindi utakapoanza kutumika.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita Nicholaus Kasendamila amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kulinda na kutunza miundombinu ya mradi huo amesema changamoto ya ukosefu wa maji imekuwa ikiwalazimu baadhi ya wananchi wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Victoria kwenda ziwani kutafuta maji na kuhatarisha maisha yao kutokana na mashambulizi ya mamba.

Kwa upande wake Diwani wa eneo linalonufaika na mradi huo amesema kukamilika kwa mradi kutapunguza kwa kiasi kikubwa adha ya wananchi kutafuta maji kwa umbali mrefu huku akiiomba Serikali kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati kama ilivyoelekezwa na Waziri.
Baadhi ya wananchi waliozungumza baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo wameishukuru Serikali kwa uwekezaji huo wamesema upatikanaji wa maji safi na salama utasaidia kuboresha afya, shughuli za kiuchumi na maisha yao kwa ujumla.