Storm FM

RC Mnyeti atoa siku 14 wananchi walipwe hela zao Mbogwe

21 September 2026, 6:47 pm

Seleman Mgunda miongoni mwa wananchi wanaoidai pesa Halmashauri ya wilaya ya Mbogwe. Picha na Mrisho Sadick

Zaidi ya wananchi watatu wamejitokeza mbele ya mkuu wa mkoa wa Geita kutoa malalamiko yao ya madai ya fedha kwa Halmashauri baada ya kutekeleza miradi ya maendeleo.

Na Mrisho Sadick:

Mkuu wa Mkoa wa Geita Alexander Mnyeti ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe kuhakikisha inalipa madeni inayodaiwa na wananchi waliotekeleza kandarasi mbalimbali za ujenzi katika miradi ya afya na elimu ndani ya halmashauri hiyo.

Mnyeti ametoa agizo hilo kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe baada ya wananchi kujitokeza na kueleza kero zao katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Lulembela.

Wananchi wa kijiji cha Lulembea wakiwa kwenye mkutano wa mkuu wa mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Miongoni mwa wananchi walioeleza changamoto hiyo ni Selemani Mgunda ambaye amesema alijenga baadhi ya majengo katika Kituo cha Afya Lulembela lakini hakulipwa fedha zake kwa wakati.

Mgunda ameeleza kuwa alilazimika kuuza nyumba yake ili kupata fedha za kuwalipa watu aliowaajiri katika utekelezaji wa ujenzi huo baada ya suala hilo kufikishwa mahakamani na kuamriwa kuwalipa.

Mkuu wa Mkoa wa Geita Alexander Mnyeti akiwa kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Lulembela. Picha na Mrisho Sadick

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbogwe Edwin Bayona baada ya kufanya uchunguzi kuhusu malalamiko hayo alibaini kuwa baadhi ya wananchi waliodai malipo hawakuwa na taarifa zao katika kumbukumbu za halmashauri, licha ya kudai kuwa walishiriki katika utekelezaji wa kazi hizo.

Kutokana na malalamiko hayo Mkuu wa Mkoa wa Geita Alexander Mnyeti amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo kuhakikisha changamoto hizo zinapatiwa ufumbuzi na madeni husika yanashughulikiwa ndani ya siku 14.

Ripoti ya Stori hii na Mrisho Sadick