Storm FM

Maombi auawa kisa elfu 10 Nyarugusu

15 November 2026, 4:31 pm

Kamanda wa Polisi Mkoa w Geita akizungumzia tukio la mauaji ya Ramadhani Maombi. Picha na Mrisho Sadick

Mzozo uliibuka baina yao ndipo Fred alimjeruhi Ramadhani kwa kitu chenye ncha kali.

Na Mrisho Sadick:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Geita limemkamata na linaendelea kumhoji Fred Andrea (32) kwa tuhuma za mauaji ya Ramadhani Maombi (34) aliyefariki katika Kituo cha Afya cha Nyarugusu akipatiwa matibabu baada ya kujeruhiwa tumboni kwa kitu chenye ncha kali.

Tukio hilo limetokea Novemba 14, 2026 majira ya saa tano na nusu usiku katika Mgahawa wa Ikoma uliopo katika Kijiji na Kata ya Nyarugusu Wilaya ya Geita.

Mtuhumiwa na marehemu walikuwa wapishi katika mgahawa huo inadaiwa kuwa baada ya kazi siku hiyo Ramadhani alimfuata Fred na kumdai shilingi 10,000 alizokuwa amemkopesha muda mrefu.

Baada ya tukio hilo mtuhumiwa alikimbia na kujificha kukwepa mkono wa sheria, Jeshi la Polisi lilimfuatilia na kumkamata akiwa mafichoni, Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani halitasita kuchukua hatua kali za kisheria kwa wanaojihusisha na vitendo hivyo.