Storm FM
Storm FM
23 November 2026, 12:45 pm

Upatikanaji wa huduma za afya ni muhimu kwa kila mwananchi bila kujali hali yake ya kiuchumi au uwezo wake wa kumudu gharama za matibabu.
Mrisho Sadick:
Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita Dkt. Khamis Mkanachi amesisitiza kuwa wananchi wasio na vyeti vya kuzaliwa au vitambulisho vya Taifa hawapaswi kunyimwa fursa ya kusajiliwa katika mpango wa Bima ya Afya kwa Wote akieleza kuwa ukosefu wa nyaraka hizo haupaswi kuwa kikwazo kwa mwananchi kupata huduma za afya kupitia mpango huo.
Dkt. Mkanachi ametoa msisitizo huo wakati wa uzinduzi wa awamu ya tatu ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote kwa kaya zilizo nje ya mpango wa TASAF wilayani Nyang’hwale uzinduzi uliofanyika katika viwanja vya Sabasaba na kuhudhuriwa na viongozi wa kitaifa wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT).
Amesema upatikanaji wa huduma za afya ni muhimu kwa kila mwananchi bila kujali hali yake ya kiuchumi au uwezo wake wa kumudu gharama za matibabu, hivyo ni muhimu kuhakikisha kuwa changamoto za ukosefu wa nyaraka za utambulisho hazizuii wananchi kunufaika na mpango huo.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Nevelin Hezron amesema utekelezaji wa awamu zilizopita umeonesha mwitikio wa wananchi katika kujiunga na mpango huo akibainisha kuwa katika awamu ya pili jumla ya kaya 1,068 zilifanikiwa kusajiliwa.
Amesema mafanikio hayo yanaonesha umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu manufaa ya kuwa na bima ya afya hususan katika kupunguza mzigo wa gharama za matibabu pale wanapohitaji huduma za afya.

Katika kuunga mkono juhudi za kupanua wigo wa wananchi wanaonufaika na mpango huo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT) Taifa Sheikh Alhad Mussa Salum amesema jumuiya hiyo imechangia usajili wa kaya 20 kama sehemu ya kuunga mkono jitihada za serikali katika kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata huduma za afya.
Amesema mchango huo ni sehemu ya dhamira ya jumuiya katika kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuboresha ustawi wa wananchi, hususan katika sekta ya afya ambayo ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii.