Storm FM

Aliyejenga jengo la wagonjwa wa nje Lulembela alipwa fedha zake

12 October 2026, 1:14 pm

Selemani Mgunda ni mmoja wa mafundi waliyokuwa wakiidai halmashauri ya wilaya ya Mbogwe. Picha na Mrisho Sadick

Mafundi hao waliibua madai hayo Septemba 19,2026 katika mkutano wa hadhara wa mkuu wa mkoa wa Geita kwenye kijiji chao cha Lulembela.

Na Mrisho Sadick:

Selemani Mgunda Mkazi wa Kijiji cha Lulembela wilayani Mbogwe Mkoani Geita aliyejenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD) katika kituo cha afya Lulembela wilayani humo nakushindwa kulipwa sehemu ya fedha hizo shilingi milioni 2.8 kwa kipindi cha miaka minne hatimaye amelipwa fedha zake baada ya mkuu wa mkoa wa Geita Alexander Mnyeti kuingilia kati.

Mgunda alitoa malalamiko hayo katika mkutano wa hadhara wa mkuu wa mkoa wa Geita Alexander Mnyeti Septemba 19,2026 Kijijini humo ambapo alisema aliingia mkataba wa ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje na halmashauri ya wilaya ya Mbogwe kwa mkataba wa shilingi milioni 9.25 akalipwa kiasi cha fedha hizo na akabaki akidai kiasi cha shilingi milioni 2.8 ambayo ameidai kwa kipindi cha miaka minne bila mafanikio.

Wananchi wa Kijiji cha Lulembela wakiwa kwenye mkutano wa mkuu wa mkoa wa Geita. Picha na Mrisho Sadick

Mkuu wa Mkoa wa Geita Alexander Mnyeti baada ya kusikiliza malalamiko hayo alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo kumlipa fedha zake Seleman Mgunda ndani ya siku 14 hatimaye fundi huyo amelipwa fedha zake zote baada ya maagizo hayo.

Sambamba na Mgunda mafundi wengine watano ambao nao walitoa malalamiko ya madai ya fedha za utekelezaji katika miradi ya serikali wilayani Mbogwe nao wamelipwa fedha zao , akizungumza na Storm FM Selemani Mgunda baada ya kulipwa fedha hizo kwa niaba ya wenzake amesema kwa pamoja walipwa zaidi ya milioni sita huku wakimshukuru mkuu wa mkoa wa Geita kwa kuingilia kati suala hilo.

Mkuu wa mkoa wa Geita akiwa kwenye mkutano katika kijiji cha Lulembela wilayani Mbogwe. Picha na Mrisho Sadick

Taarifa zaidi na Mrisho Sadick