Storm FM
Storm FM
1 September 2026, 2:02 pm

Mahitaji ya nyanya yamekuwa makubwa wilayani Geita huku wakulima wakitakiwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mbogamboga hali ambayo itasaidia kuwawezesha wakulima kuongeza kipato na kukidhi mahitaji ya soko
Na Mrisho Sadick:
Wakulima wa mbogamboga wilayani Geita mkoani Geita wametakiwa kutumia fursa ya kilimo cha nyanya kuongeza uzalishaji na kipato kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya zao hilo ndani na nje ya Tanzania.
Mkuu wa Wilaya ya Geita Hashim Komba ametoa rai hiyo wakati wa uzinduzi wa kitalu cha Raha Vegetable Farm kinachozalisha miche ya nyanya hoho na pilipili mwendokasi katika Kata ya Nyamigota wilayani Geita.

Amesema kuongezeka kwa mahitaji ya mazao hayo kunatoa fursa kubwa kwa wakulima kuongeza uzalishaji na kujenga kipato endelevu huku akiwataka kutumia teknolojia na pembejeo bora ili kuongeza tija katika kilimo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Pembejeo za Kilimo AGITF, Mwanahiba Mohamed Mzee amesema mfuko huo umeendelea kuwezesha upatikanaji na matumizi ya pembejeo bora za kilimo sambamba na kuwawezesha wadau kupata huduma za kifedha zinazohusiana na uzalishaji wa kilimo.

Naye Mkurugenzi wa Raha Vegetable Farm Raha Aloyce amesema Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya kampuni hiyo, baada ya kuiwezesha kupata mkopo uliosaidia kuanzisha vitalu vya kisasa vya uzalishaji wa miche katika maeneo mbalimbali nchini.