Storm FM

Wananchi wadai kushambuliwa na fisi nyakati za usiku Ngoma

2 September 2026, 4:09 pm

Wanyama aina ya fisi wanaodaiwa kusumbua wananchi katika Kata ya Ngoma B Sengerema. Picha kutoka Mtandaoni

Wakati Serikali ikiendelea na jitihada za kukabiliana na fisi hao, wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari, ikiwemo kuepuka kutembea katika maeneo hatarishi nyakati za usiku.

Na Mrisho Sadick:

Wananchi wa Kata ya Ngoma B, Wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza, wameiomba Serikali kuingilia kati suala la fisi wanaodaiwa kuvamia maeneo ya makazi na kuwashambulia wananchi katika kata hiyo.

Wananchi hao wamesema hali hiyo imezua hofu kubwa miongoni mwao, huku baadhi wakieleza kuwa sasa wanaishi kwa wasiwasi kutokana na vitisho vinavyosababishwa na uwepo wa wanyama hao katika maeneo yao.

Wamesema mashambulizi hayo yamekuwa yakihatarisha usalama wao, hususan nyakati za usiku, na kuathiri shughuli zao za kila siku kutokana na hofu ya kukutana na fisi wanapotoka au kurejea katika makazi yao.

Wameiomba Serikali kupitia mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kudhibiti wanyama hao, ili kurejesha hali ya usalama na kuwawezesha kuendelea na shughuli zao bila hofu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Mheshimiwa Senyi Nganga, amesema Serikali imelipokea suala hilo na inaendelea kulifanyia kazi kwa kushirikiana na mamlaka zinazohusika na uhifadhi na udhibiti wa wanyamapori.

Ripoti kamili ya Stori hii na Mrisho Sadick