Storm FM

GGML yawakumbusha wanahabari kuendelea kuzingatia weledi

15 September 2026, 11:54 am

Mkufunzi mwandishi mwandamizi Sammy Awami akizungumza na wana habari (hawapo picha). Picha na mpiga picha wetu

“Jamii inapopata taarifa sahihi kutoka vyanzo vya uhakika inasaidia kuchochea maendeleo kwenye jamii na kuendeleza uhusiano bora na wenye tija kati ya serikali na wawekezaji” – Simon Shayo, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti inayomiliki GGML

Na: Ester Mabula

Mgodi wa Dhahabu wa Geita (GGML) umeeleza kuwa utaendelea kushirikiana na vyombo vya habari vyote nchini ili kuwezesha utoaji wa taarifa wenye tija kwa maslahi ya UMMA.

Hayo yamebainika katika mafunzo kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Kengo Limited, kwa niaba ya Geita Gold Mining Limited (GGML) yakihusisha waandishi wa habari kutoka mkoani Geita.

Awali akifungua mafunzo hayo kwa njia ya mtandao (zoom meeting) Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti inayomiliki GGML Ndg. Simon Shayo amesema wanathamini vyombo vya habari kwani ni wadau muhimu katika utendaji wao na kwamba wataendelea kushirikiana na taasisi zote za binafsi na serikali ili kuwezesha utoaji wa taarifa sahihi zitakazosaidia kuchochea ushirikiano wenye tija katika shughuli za uwekezaji na maendeleo kwa ujumla.

Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma GGML, Stephen Mhando akizungumza na wana habari (hawapo pichani). Picha na mpiga picha wetu

Meneja wa Mawasiliano na Mahusiano kwa Umma GGML, Stephen Mhando amesema GGML kupitia kitengo cha mahusiano kwa UMMA imejizatiti kuendeleza ushirikiano ili kuwezesha upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu shughuli zake.

Mkufunzi  katika warsha hiyo, Mwandishi Mwandamizi Sammy Awami amesisitiza waandishi wa habari kuzingatia misingi ya kitaaluma akieleza kuwa uhabarishaji wenye tija ni ule unaozalisha habari zenye mvuto kwa hadhira pasipo kukiuka misingi ya kitaaluma kwa kuhusisha vyanzo sahihi pasipo kuegemea upande mmoja.

Baadhi ya washiriki Ester Mabula kutoka Storm FM na Yohana Shida kutoka Habari Leo wakiwa katika mafunzo. Picha na mpiga picha wetu

Baadhi ya waandishi wa habari walioshiriki katika mafunzo hayo akiwemo Edga Rwenduru kutoka EATV/EA Radio, Agnes Kilala kutoka Rubondo FM na Yohana Shida kutoka Habari Leo/Daily News  wamepongeza uwepo wa mafunzo hayo na kueleza kupitia mafunzo hayo wataendelea kuzingatia weledi katika uhabarishaji wa taarifa kwa Jamii.

Waandishi wa habari, watendaji kutoka Kengo Ltd na GGML wakiwa katika picha ya pamoja baada ya mafunzo. Picha na mpiga picha wetu