Storm FM

TANAPA yazindua shangwe la sikukuu hifadhi za taifa

21 November 2026, 12:15 pm

Watalii wa ndani kutoka maeneo mbalimbali wakiwa kwenye uzinduzi wa shangwe la sikukuu. Picha na Daniel Magwina

Kampeni hiyo inalenga kuwahamasisha Watanzania kutumia kipindi cha sikukuu kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.

Na Daniel Magwina – Geita

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) limezindua msimu wa tatu wa kampeni ya Shangwe la Sikukuu ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhamasisha utalii wa ndani katika kipindi hiki cha sikukuu.

Kupitia kampeni hiyo TANAPA imejipanga kuvipa kipaumbele na kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii ikiwemo hifadhi za taifa maeneo ya makumbusho na malikale ambayo hayajapewa kipaumbele cha kutosha kwa lengo la kuvifanya vifahamike zaidi kwa Watanzania na wageni wengine.

Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA Jully Bede Lyimo akizungumzia kampeni hiyo. Picha na Daniel Magwina

Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo mkoani Geita, Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA Jully Bede Lyimo, amesema kampeni hiyo inalenga kuwahamasisha Watanzania kutumia kipindi cha sikukuu kutembelea na kujionea vivutio mbalimbali vilivyopo nchini.

Sauti ya Mkuu wa Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA

Kwa upande wake Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo Dkt. Imani Kikoti amesema kisiwa hicho ni cha kipekee kutokana na kuwa na mazalia ya samaki pamoja na aina mbalimbali za ndege wenye muonekano na mvuto wa kipekee, hali inayokifanya kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya utalii wa asili.

Sehemu ya mandhari ya hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo. Picha na Daniel Magwina
Sauti ya Mkuu wa Kisiwa cha Rubondo

Baadhi ya watu waliopata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa cha Rubondo wameeleza kuvutiwa na mandhari yake pamoja na vivutio mbalimbali vinavyopatikana katika eneo hilo, huku wakisifu uzuri na upekee wa hifadhi hiyo na kuwataka Watanzania wengine kuitembelea ili kujionea vivutio vilivyopo.

Sauti ya Wananchi

Kampeni ya Shangwe la Sikukuu inatarajiwa kuongeza hamasa ya utalii wa ndani, kuibua mwamko wa Watanzania kutembelea hifadhi za taifa na maeneo mengine ya urithi wa taifa, pamoja na kuchangia ukuaji wa sekta ya utalii nchini.