Mazingira FM
Mazingira FM
16 November 2026, 1:29 pm

Kwa ujumla, miradi hiyo yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 747 katika sekta za afya na elimu inaonesha mchango wa ushirikiano kati ya mgodi na jamii katika kuboresha huduma za kijamii,
Na Adelinus Banenwa
Ujenzi wa nyumba za watumishi wa afya katika Kituo cha Afya Nyangoto, maabara za sayansi katika Shule ya Sekondari Nyabichune pamoja na jengo la utawala katika Shule ya Sekondari Matongo ni miongoni mwa miradi iliyotekelezwa na Mgodi wa Barrick North Mara kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), inayotajwa kusaidia kuboresha huduma za afya na elimu wilayani Tarime.
Katika sekta ya afya, mgodi huo umejenga nyumba tatu zinazotumiwa na familia tano za wahudumu wa Kituo cha Afya Nyangoto kwa gharama ya shilingi milioni 335.
Baadhi ya wananchi wameushukuru mgodi huo wakieleza kuwa kabla ya ujenzi wa nyumba hizo, wagonjwa waliokuwa wakifika kituoni hapo nyakati za usiku, wakiwemo wanawake wajawazito wanaohitaji huduma za kujifungua, walilazimika kusubiri kati ya dakika 30 hadi 45 kumpata mhudumu wa afya.

Akizungumzia manufaa ya mradi huo, Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Nyangoto, Abduladhimu Sued Ally, amesema uwepo wa nyumba hizo umesaidia watumishi kuwa karibu na eneo la kazi na kuongeza muda wa upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa, tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Katika sekta ya elimu, kupitia mpango huo wa CSR, Mgodi wa Barrick North Mara umejenga maabara tatu za masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia katika Shule ya Sekondari Nyabichune kwa gharama ya shilingi milioni 240.
Mwalimu wa shule hiyo, Patrick Michael Gabriel, amesema uwepo wa maabara hizo umesaidia kuongeza idadi ya wanafunzi wanaosoma masomo ya sayansi kutoka wanafunzi 20 mwaka 2025 hadi kufikia 41 mwaka 2026, sawa na ongezeko la wanafunzi 21.

Aidha, katika Shule ya Sekondari Matongo, mgodi huo umefanikisha ujenzi wa jengo la utawala kwa gharama ya shilingi milioni 172, hatua inayolenga kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa walimu na usimamizi wa shughuli za shule.
Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Boniface Masunga Shagembe, amesema uwepo wa jengo hilo umewawezesha walimu kupata ofisi na sehemu salama ya kuhifadhi nyaraka mbalimbali za shule, ikiwemo nyaraka za siri.
Amesema kabla ya ujenzi wa jengo hilo, walimu walikuwa wakitumia chumba cha darasa kama ofisi, hali iliyokuwa ikileta changamoto katika utendaji kazi na uhifadhi wa nyaraka muhimu.
Kwa upande wa ushirikiano kati ya jamii na mgodi, Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii na Mgodi (CDC) Bogomba, Rashidi amesema wanaendelea kuimarisha mahusiano baina ya wananchi na Mgodi wa Barrick North Mara kwa kushirikiana katika kutatua changamoto zinazojitokeza kati ya pande hizo mbili.
Hata hivyo, ameitaka jamii, hususan vijana, kujiepusha na shughuli za uchimbaji katika maeneo yaliyo ndani ya leseni ya mwekezaji, akisisitiza umuhimu wa kulinda ushirikiano uliopo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kushirikiana na Mgodi wa North Mara na kujiepusha na vitendo vya hujuma, ikiwemo kufanya shughuli za uchimbaji katika maeneo yenye leseni ya mwekezaji.
Amesema vitendo hivyo vinaweza kuathiri uzalishaji wa mgodi na kusababisha kupungua kwa mapato yanayoweza kuchangia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).
Kwa ujumla, miradi hiyo yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 747 katika sekta za afya na elimu inaonesha mchango wa ushirikiano kati ya mgodi na jamii katika kuboresha huduma za kijamii, huku wadau wakihimizwa kuendeleza mahusiano hayo kwa manufaa ya maendeleo ya wananchi.