Mazingira FM

Tarime yaandaa kambi salama kuwanusuru watoto dhidi ya ukeketaji

28 September 2026, 9:11 pm

Pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mhe. Meja Edward Gowele (aliyekaa katikati mwenye suti nyeusi) pembeni yake mkono wa kulia ni Mwenyekiti wa Safe Society Platform Tanzania (Jukwaa la Jamii Salama ) wakiwa katika kikao cha kujadili mipango ya ‘Kambi Salama’

Hatua hiyo inalenga kuhakikisha watoto wanaokimbia ukeketaji hawakosi sehemu salama ya kwenda

Na Edward Lucas.

Wadau wa kupinga ukeketaji wilayani Tarime mkoani Mara wameandaa mpango wa kuanzisha kambi salama ya muda kwa ajili ya kuwahifadhi watoto wa kike watakaokimbia ukeketaji katika kipindi cha msimu wa vitendo hivyo unaotarajiwa kuanza katika miezi ya Oktoba hadi Desemba mwaka huu.

Mpango huo umeandaliwa na Safe Society Platform Tanzania (Jukwaa la Jamii Salama) kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tarime , Ustawi wa Jamii na wadau wengine, baada ya kutokuwepo kwa sasa kwa Nyumba Salama ya Masanga iliyokuwa miongoni mwa maeneo yaliyotumiwa kuwahifadhi watoto wanaokimbia ukeketaji.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Safe Society Platform Tanzania, Jacob Sira Matiko, hatua hiyo inalenga kuhakikisha watoto wanaokimbia ukeketaji hawakosi sehemu salama ya kwenda, huku kambi hiyo ikitarajiwa kufanya kazi kwa kipindi cha muda wakati wa msimu wa ukeketaji.

Sauti ya Jacob Sira Matiko

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, amesema pamoja na kuwa na maeneo salama ya kuwahifadhi watoto, jamii inapaswa kuimarisha elimu na ushirikiano na wazee wa kimila katika koo zinazohusishwa na vitendo hivyo.

Amesema hatua nyingine ni kuwawezesha baadhi ya mangariba na wazee wa kimila kupata shughuli mbadala za kiuchumi, kutokana na kuwepo kwa baadhi yao wanaonufaika na ukeketaji.

Sauti ya Mhe. Meja Edward Gowele

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Mji wa Tarime, Fatna Maneno, amesema elimu endelevu ni muhimu katika kukabiliana na ukeketaji, huku akieleza kuwa baadhi ya watu wanaotoa elimu dhidi ya vitendo hivyo wamewahi kukabiliwa na vitisho.

Sauti ya Fatna Maneno
Miongoni mwa wadau muhimu wakichangia mikakati mbalimbali kuhakikisha watoto wa kike wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukeketaji

Wakati huo huo, Balozi wa Kampuni ya Soya One Limited, Fredrizo Samson, amesema kampuni hiyo imechangia shilingi milioni 1.5 kusaidia mahitaji ya watoto watakaohifadhiwa katika kambi hiyo, akisisitiza umuhimu wa elimu dhidi ya ukeketaji kutolewa mapema na kuendelea mwaka mzima.

Wadau hao wameendelea kusisitiza umuhimu wa jamii, serikali, mashirika na taasisi mbalimbali kushirikiana katika kulinda watoto dhidi ya ukeketaji, huku kambi hiyo ikitarajiwa kuwa sehemu ya hatua za muda za kuwapatia usalama watoto watakaokimbia vitendo hivyo.