Mazingira FM
Mazingira FM
20 October 2026, 7:11 pm

Tumejiandaa pia kujifunza kutoka kwa washiriki wengine ili kupata maarifa yatakayosaidia kuboresha shughuli zetu
Na Adelinus Banenwa
Shirika la BUFADESO limewahimiza wakazi wa Mkoa wa Mara kujitokeza kwa wingi kutembelea Kongamano na Maonesho ya 11 ya Kilimo Misitu yanayoendelea katika eneo la VI Agroforestry, Bweri, wilayani Musoma, kuanzia Oktoba 19 hadi 21, 2026.
Akizungumza katika maonesho hayo, Mwanaidi Marwa, mnufaika kutoka BUFADESO, amesema shirika hilo limejipanga kuwahudumia wananchi watakaotembelea banda lao kwa kuwaonesha bidhaa mbalimbali zinazotokana na uongezaji wa thamani wa malighafi za kilimo na mifugo.

Amesema kuwa, pamoja na kuonesha bidhaa hizo, wamejiandaa pia kujifunza kutoka kwa washiriki wengine ili kupata maarifa yatakayosaidia kuboresha shughuli zao.
Kwa upande wake, Granta Marwa, mwakilishi kutoka taasisi ya TABIO, amesema taasisi hiyo imeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu kwa jamii kuhusu mazao ya asili yaliyo katika hatari ya kutoweka.

Amesema TABIO ina jukumu la kukusanya, kuhifadhi na kusambaza mbegu za mazao hayo ili kuhakikisha yanaendelea kuwepo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Baadhi ya mazao hayo ni mchecha lishe wa asili, maharage ya asili yanayochukua hadi siku 240 kukomaa, pamoja na mboga ya asili inayojulikana kama msusa, miongoni mwa mazao mengine.
Maonesho hayo yamefunguliwa Oktoba 19, 2026, na yanatarajiwa kuhitimishwa Oktoba 21, 2026, yakilenga kutoa fursa kwa wananchi kujifunza kuhusu kilimo, misitu, uhifadhi wa mbegu za asili na uongezaji wa thamani wa mazao ya kilimo na mifugo.