Mazingira FM
Mazingira FM
26 September 2026, 7:03 pm

Dk. Bwire ameahidi kutoa zawadi kwa kila mwalimu atakayefanikisha wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Isanju kupata alama A 20 kwa kila somo.
Na Adelinus Banenwa
Dk. Masinde Bwire ameahidi kushirikiana na uongozi wa Shule ya Msingi Isanju, iliyopo Kata ya Iramba, wilayani Bunda, katika kuboresha mazingira ya shule hiyo kwa kusaidia ujenzi wa matundu mawili ya vyoo, kutoa kompyuta mbili, pamoja na mabati na misumari kwa ajili ya kukamilisha nyumba ya mwalimu.
Dk. Bwire ametoa ahadi hiyo wakati akiwa mgeni rasmi katika mahafali ya Darasa la Saba ya mwaka 2026 yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Isanju.
Aidha, amewahimiza wanafunzi kuzingatia elimu na kuitumia ipasavyo, akieleza kuwa elimu ni miongoni mwa nyenzo muhimu za kuwawezesha kujikwamua na kuboresha maisha yao.

Katika risala ya wahitimu pamoja na taarifa ya shule, imeelezwa kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo uchakavu wa baadhi ya majengo, ukosefu wa vyoo vya walimu, upungufu wa matundu ya vyoo kwa wanafunzi, pamoja na upungufu wa nyumba za walimu.
Kwa upande mwingine, katika jitihada za kuchochea ufaulu na kuwapa motisha walimu, Dk. Bwire ameahidi kutoa zawadi kwa kila mwalimu atakayefanikisha wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Isanju kupata alama A 20 kwa kila somo.
Amesema hatua hiyo inalenga kuhamasisha walimu kuongeza juhudi katika ufundishaji na kusaidia kupandisha kiwango cha ufaulu wa wanafunzi katika shule hiyo.