Mazingira FM
Mazingira FM
24 September 2026, 7:58 pm

Hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto na migogoro kwa wananchi, hususan migogoro inayoweza kutatuliwa kupitia vikao na mikutano ya kiserikali.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge, ameelekeza kamati zote kuanzia ngazi ya serikali za mitaa hadi halmashauri kuhakikisha zinafanya mikutano yote kwa wakati, kwa mujibu wa kalenda na ratiba zilizowekwa.
Mhe. Kaminyoge amesema hatua hiyo inalenga kupunguza changamoto na migogoro kwa wananchi, hususan migogoro inayoweza kutatuliwa kupitia vikao na mikutano ya kiserikali.
Mkuu huyo wa Wilaya ametoa maelekezo hayo leo katika Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Mji wa Bunda, lililoketi kujadili taarifa za robo ya nne ya mwaka wa fedha 2025/2026.

Aidha, Mhe. Kaminyoge ameiagiza Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuhakikisha inafanya jitihada za kusafisha mitaro na mifereji ya maji, ikiwa ni sehemu ya maandalizi na tahadhari dhidi ya athari zinazoweza kujitokeza kutokana na mvua za El NiƱo.
Kwa niaba ya Meneja wa TARURA Wilaya ya Bunda, Mhandisi Hamedi Munisi, amesema TARURA tayari inaendelea na kazi ya kuzibua mitaro pamoja na kusafisha maeneo yanayoweza kuwa kikwazo kwa mtiririko wa maji.
Amesema kazi hiyo inalenga kuhakikisha maji yanapata njia ya kupita, hasa katika maeneo yenye mikondo mikubwa ya maji, ili kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.