Mazingira FM
Mazingira FM
15 September 2026, 9:48 pm

Dereva anaweza kupata nukta moja kwa kosa la kutofunga mkanda wa usalama, nukta tatu kwa kosa la uendeshaji wa hatari na nukta tano kwa kosa la mwendokasi
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa Usalama Barabarani Wilaya ya Bunda, ASP Faustine Buhembere, amewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, hususan mfumo wa upunguzaji wa nukta (point) kwenye leseni za udereva, ili kuepuka kufungiwa leseni zao.
Akizungumza kupitia Redio Mazingira FM katika kipindi cha asubuhi leo, ASP Buhembere amesema madereva wanapaswa kufahamu kuwa makosa mbalimbali ya barabarani yanaweza kusababisha kupunguzwa kwa nukta kwenye leseni zao, kulingana na uzito wa kosa.
Mfumo huo unatokana na Sheria ya Usalama Barabarani, Sura ya 168, ambapo kanuni za uwekaji wa nukta kwenye leseni zilianzishwa ili kuimarisha uzingatiaji wa sheria na usalama barabarani.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, dereva anaweza kupata nukta moja kwa kosa la kutofunga mkanda wa usalama, nukta tatu kwa kosa la uendeshaji wa hatari na nukta tano kwa kosa la mwendokasi. Nukta zinapofikia 15, leseni ya dereva hufungiwa kwa kipindi cha miezi sita.
ASP Buhembere amewataka madereva kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepuka makosa yanayoweza kusababisha kupungukiwa nukta na hatimaye kufungiwa leseni zao.