Mazingira FM

Nyasura: tutapita nyumba kwa nyumba wanafunzi wote waende shule.

14 February 2023, 11:06 am

Uongozi wa Kata ya Nyasura Halmashauri ya Mji wa Bunda Mkoani Mara umeweka mikakati ya kupita nyumba hadi nyumba kuhakikisha watoto wote waliopaswa kuwa shule waweze kufika shule kwa wakati.

Hayo yamebainishwa leo na Afisa Mtendaji wa kata Hiyo, Bi Jonmary Athanasi Kamgisha alipokuwa anafanya mahojiano na Mazingira Fm katika ofisi za serikali ya mtaa wa Nyasura D wakati wa zoezi la kukabidhi vifaa vya shule kwa mwanafunzi Baraka Samweli vilivyotolewa na Kikundi cha Tupendane kinachopatikana Nyasura.

Bi Jonmary Athanasi Kamgisha amesema kwa kata ya Nyasura wana shule moja tu ya Sekondari ya Dr Nchimbi ambapo hadi sasa wamekwisha ripoti wanafunzi 500 kati ya wanafunzi 567 waliopangwa kidato cha kwanza kwa mwaka huu 2023 hivyo uongozi unaweka mipango kuhakikisha wanafunzi wote wa shule za msingi na wale waliopangwa kidato cha kwanza wanakwenda shule kwa wakati.