Mazingira FM
Mazingira FM
17 June 2026, 6:45 pm

Tukio lililotokea wakati mwanafunzi huyo alipokwenda eneo hilo kwa ajili ya kuchota maji majira ya saa tisa alasiri.
Na Adelinus Banenwa
Mtoto Waryoba Sungura (11), mwanafunzi wa darasa la tatu katika Shule ya Msingi Butimba iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, amepoteza maisha baada ya kuzama kwenye dimbwi la maji lililoachwa wazi kufuatia zoezi la uchimbaji changarawe katika Kijiji cha Butimba,
Kwa mujibu wa Sungura Maiso Misanda baba mzazi wa mtoto huyo amesema tukio lililotokea wakati mwanafunzi huyo alipokwenda eneo hilo kwa ajili ya kuchota maji majira ya saa tisa alasiri ndipo baadaye walipopata taarifa ya kuzama kwa mtoto wao.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Butimba ameeleza kuwa eneo hilo liliachwa wazi baada ya kukamilika kwa zoezi la uchimbaji wa changarawe kutokana na maombi ya wananchi wenyewe walioomba lisifukiwe ili walitumie kwa ajili ya kunywesha mifugo yao pamoja na kupata maji ya matumizi mengine ya nyumbani.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo amebainisha kuwa hili si tukio la kwanza la watoto kuzama katika dimbwi hilo kwani huko nyuma watoto wanne waliwahi kutumbukia ambapo wawili walinusurika na wengine wawili walipoteza maisha, hali iliyomfanya kutoa wito wa dharura kwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) kulifukia shimo hilo haraka ili kunusuru maisha ya watoto wengine.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Butimba amesema kuwa tukio hilo limeacha simanzi na majonzi makubwa katika jamii, na akasisitiza kuwa kwa sasa uongozi wa kata unashirikiana kwa karibu na familia ya marehemu katika maandalizi ya kuupumzisha mwili wa mtoto huyo baada ya Jeshi la Polisi kukamilisha taratibu zake na kuukabidhi kwa ndugu.