Mazingira FM

Uwezeshwaji wachangia kuinua wanawake kiuchumi Bunda

18 August 2026, 11:09 pm

Moja ya akina mama kikundi cha USHIRIKIANO Kibara

Mafanikio ya kikundi yamewafanya wanachama pia kuanza kuwa na biashara binafsi. Kila mwanachama alipewa shilingi laki nane kwa ajili ya kuanzisha au kukuza biashara yake.

Na Edward Lucas

Kutoka katika biashara ndogo za kuuza nyanya, mbogamboga na matunda, hadi kuwa na shughuli ya upishi yenye mtaji wa zaidi ya shilingi milioni 40, ni mabadiliko yanayoshuhudiwa na kikundi cha wanawake Ushirikiano kutoka kijiji cha Kibara, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Wanawake hao walianza kama kikundi cha kuweka na kukopa mwaka 2021, kabla ya kuanza kunufaika na mikopo ya Halmashauri mwaka 2024 kupitia shughuli za upishi misiba, mikutano, sherehe na matukio mengine ya jamii.

Sauti ya Zenaeda Charles Palapala, Mwenyekiti

Kupitia mikopo hiyo, ambayo wamekuwa wakipata kwa awamu tofauti, wanawake hao wameweza kukuza shughuli ya upishi na kufikisha mtaji wa kikundi zaidi ya shilingi milioni 40.

Kwa sasa, kikundi kinaweza kupata kati ya shilingi laki tatu hadi laki nane kwa kila kazi, huku mapato hayo yakisaidia mahitaji ya wanakikundi na familia zao.

Sauti ya Leticia Pastory Majura, Mwanakikundi

Mafanikio ya kikundi yamewafanya wanachama pia kuanza kuwa na biashara binafsi. Kila mwanachama alipewa shilingi laki nane kwa ajili ya kuanzisha au kukuza biashara yake.

Leticia alitumia fedha hizo kuanzisha duka la nguo baada ya mumewe kumuongezea shilingi laki mbili.

Sauti ya Leticia Pastory Majura

Kwa mwenyekiti wa kikundi hicho, uwezeshaji huo umeongeza uwezo wa wanawake kuchangia mahitaji ya familia, tofauti na zamani ambapo familia nyingi zilimtegemea mtu mmoja.

Sauti ya Zenaeda Charles Palapala

Pamoja na mafanikio hayo, wanawake hao bado wanakabiliwa na changamoto ya kupata mikopo pungufu ya kiasi wanachoomba, jambo linalochelewesha baadhi ya malengo yao.

Kwa upande wa Halmashauri, Kaimu Mkuu wa Maendeleo ya Jamii Bunda DC, Octavina Kiwone, anasema uwezeshaji kupitia mikopo unaendelea na katika mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ilitoa jumla ya shilingi milioni 439.5 kwa vikundi vya makundi hayo, ikiwa ni zaidi ya lengo la shilingi milioni 320.174.