Mazingira FM

Ukeketaji unavyochangia ndoa za utotoni

23 August 2026, 3:22 pm

Asilimia 38.3 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 mkoani Mara walikuwa wameolewa kabla ya kufikisha miaka 18.

Na Edward Lucas

Baadhi ya mila zinazohusisha ukeketaji mkoani Mara zimeelezwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia wasichana kuingia kwenye ndoa wakiwa na umri mdogo, huku baadhi ya ngariba wakisema ukeketaji umeendelea kuhusishwa na maandalizi ya mtoto wa kike kuolewa.

Mzee Maro Kerindo, mkazi wa Serengeti na aliyewahi kuwa ngariba, amesema katika baadhi ya jamii mafanikio ya ngariba yamekuwa yakipimwa kwa kuangalia idadi ya wasichana aliowafanyia ukeketaji ambao baadaye wameolewa na kupata watoto.

Sauti ya Maro Kerindo

Rhobi John, aliyewahi kuwa ngariba katika Wilaya ya Tarime, amesema ukeketaji kwa sasa unafanyika hata kwa wasichana wenye umri wa miaka 11 na 12, huku baadhi ya familia zikihusisha kubalehe na maandalizi ya ndoa.

Sauti ya Rhobi John

Rhobi amesema katika baadhi ya jamii, mtoto wa kike anapobalehe familia huanza kutafuta namna ya kumuozesha ili asije akapata ujauzito akiwa nyumbani, hali inayoweza kusababisha ukeketaji kufanyika akiwa bado mtoto.

Wakati huo huo, Mzee Kerindo amesema umaskini na mahitaji ya familia pia vinaweza kuchangia watoto kuingizwa kwenye makubaliano ya ndoa wakiwa wadogo, ambapo wakati mwingine mali hutolewa bila mtoto mwenyewe kufahamu.

Sauti ya Rhobi John

Takwimu za Tanzania Demographic and Health Survey za mwaka 2022 zinaonesha kuwa asilimia 28 ya wanawake wenye umri wa miaka 15 hadi 49 mkoani Mara wamewahi kufanyiwa ukeketaji.

Aidha, asilimia 38.3 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 hadi 24 mkoani Mara walikuwa wameolewa kabla ya kufikisha miaka 18, ikilinganishwa na asilimia 29.1 kwa Tanzania nzima.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, jamii imetakiwa kuimarisha elimu, kuwalinda watoto na kuwawezesha kiuchumi wazazi pamoja na ngariba wanaoachana na vitendo vya ukeketaji.