Mazingira FM
Mazingira FM
8 September 2026, 8:51 pm

Mkoa wa Mara una jumla ya watahiniwa 59,995 kutoka shule 939 wanaotarajiwa kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi,
Na Adelinus Banenwa
Mkoa wa Mara una jumla ya watahiniwa 59,995 kutoka shule 939 wanaotarajiwa kufanya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi, unaofanyika kwa siku mbili, Septemba 9 na 10, 2026.
Dkt. Elpidius Baganda Afisa elimu Mkoa wa Mara amesema kati ya watahiniwa hao, wasichana ni 31,272 na wavulana 28,723, huku akiwaonya kujiepusha na udanganyifu, ikiwemo kuingia na simu janja, saa janja au vikaratasi vya majibu katika vyumba vya mitihani.
Amesema hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya atakayebainika kufanya udanganyifu.
Kwa upande wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, shule 71 zitafanya mtihani huo, zikiwemo shule 63 za Serikali na nane za binafsi, zenye jumla ya watahiniwa 5,391; wavulana 2,630 na wasichana 2,761.
Afisa Elimu Awali na Msingi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mwal Saidi Jumanne Ramadhani, amesema maandalizi yote yamekamilika, ikiwemo kuwasambaza wasimamizi katika vituo vyao.
Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Profesa Said Mohamed, jumla ya watahiniwa 1,168,649 kutoka Tanzania nzima wanatarajiwa kufanya mtihani huo.