Mazingira FM
Mazingira FM
9 September 2026, 3:24 pm

Madereva hao pia wametoa wito kwa vituo vingine vya madereva bodaboda kuwa na utamaduni wa kufanya usafi mara kwa mara katika maeneo yanayowazunguka.
Na Adelinus Banenwa
Maafisa usafirishaji maarufu kama madereva wa bodaboda katika Kituo cha Diamond, Bunda Mjini, wameiomba Serikali na mamlaka husika kuchukua hatua dhidi ya watu na wafanyabiashara wanaotupa taka ovyo kwenye mitaro.
Madereva hao wamesema tabia hiyo imekuwa ikisababisha mitaro kuziba, hali inayochangia uchafuzi wa mazingira pamoja na kuwepo kwa harufu kali na kero kwa wananchi wanaotumia maeneo hayo.
Wametoa rai hiyo leo, Septemba 9, 2026, wakati wakiendelea na zoezi la usafi kwa kusafisha mitaro na makaravati yanayozunguka eneo lao la kazi.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, mwenyekiti wa kituo cha Diamond, Japhet John, amesema wameamua kufanya usafi kutokana na hali ya mazingira katika eneo hilo kutokuwa nzuri, huku harufu iliyokuwa ikitoka kwenye mitaro ikiwa imekuwa kero hata kwa baadhi ya wateja wao.

Kwa upande wao, baadhi ya madereva wa bodaboda katika kituo hicho wameiomba Serikali kuchukua hatua za kuondoa taka zilizokusanywa katika zoezi hilo, ili zisije zikawa chanzo kingine cha kero kwa wananchi kutokana na kuendelea kurundikana katika eneo hilo.
Madereva hao pia wametoa wito kwa vituo vingine vya madereva bodaboda kuwa na utamaduni wa kufanya usafi mara kwa mara katika maeneo yanayowazunguka, wakisema hatua hiyo ni muhimu katika kulinda afya zao pamoja na afya za wateja wao.

Wamesisitiza kuwa usafi wa mazingira si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha eneo analoishi au kufanyia shughuli linakuwa safi na salama.