Mazingira FM

Apanda mlingoti wa bendera akiwa uchi akishinikiza kumuona mgonjwa

9 September 2026, 9:34 pm

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku mtuhumiwa akitarajiwa kufikishwa mahakamani

Na Adelinus Banenwa

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara linamshikilia Dickson Juma, mwenye umri wa miaka 32, mkazi wa Kiabakari, Wilaya ya Butiama, kwa tuhuma za kuingia bila kibali na kufanya fujo katika Kituo cha Afya Nyasho, Manispaa ya Musoma.

Tukio hilo limetokea Septemba 9, 2026, majira ya saa 4:00 asubuhi, baada ya mtuhumiwa kufika kituoni hapo akiwa na mke na mtoto wake waliokuwa wamelazwa.

Kwa mujibu wa Polisi, baada ya kuzuiliwa na walinzi na kutakiwa kufuata taratibu za kituo hicho, mtuhumiwa alianza kufanya fujo, kuvua nguo na kupanda juu ya mlingoti wa bendera ya Taifa, akionyesha nia ya kushinikiza kuruhusiwa kuingia ndani kuwaona ndugu zake.

Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku mtuhumiwa akitarajiwa kufikishwa mahakamani baada ya taratibu za kisheria kukamilika.

Polisi Mkoa wa Mara imetoa wito kwa wananchi kuheshimu sheria, kanuni na taratibu za taasisi za umma ili kuepuka vitendo vinavyoweza kuleta usumbufu au kuwafanya wakabiliwe na hatua za kisheria.