Mazingira FM

MBUNGE ROBERT MABOTO ATOA PIKIPIKI 14 KWA KATA 14 ZA JIMBO LA BUNDA MJINI

15 July 2022, 10:43 pm

Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini Mhe. Robert Chacha Maboto amegawa pikipiki 14 kwa vikundi vya waendesha pikipiki kutoka Katika kila Kata za Halmashauri ya Mji wa Bunda ndani ya Jimbo la Bunda Mjini Leo Tarehe  15.07.2022, Uwanja wa Sabasaba.

Hii ni katika kusaidia kukabiliana na tatizo la Ajira kwa Vijana. Mheshimiwa Maboto amesema pikipiki hizo zitasaidia Vijana kujiajiri kwa kukopeshana na marejesho yatakayokua yanapatikana yatakua yakinunua pikipiki nyingine kwa watu wengine.

Mheshimiwa Maboto amesema hayo yote anayafanya kwa kutuamia mshahara wake wa ubunge. Mbunge amesisitiza pia ataendelea kufanya hayo kwa Wananchi wake wa Jimbo la Bunda Mjini na amewaahidi wanawake kwamba kabla ya Mwezi wa kumi na mbili kupitia vikundi vyao atawapatia Mtaji wa kujiendesha zaidi.

Aidha, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mara ambae pia ni mgeni rasmi katika tukio hili Mhe. Langaeli Akyoo amempongeza sana Mheshimiwa Maboto kwa uthubutu ambao anaufanya wa kuleta Maendeleo kwa wapiga kura wake kwani si wote huwa wanawakumbuka Wapiga kura wao. Amewataka wakazi wa Bunda kumuunga Mkongo Mheshimiwa Maboto Ili aweze kuleta Maendeleo ya kweli na kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.

Awali Mheshimiwa Joshua Nassari Mkuu wa Wilaya ya Bunda amewaeleza wakazi wa Jimbo la Bunda Mjini juu ya ushirikiano uliopo baina ya Viongozi wa Serikali na wa kuchaguliwa. Amesema ni mara chache sana kukuta Mbunge wa Jimbo Fulani anaongea vizuri na Mkuu wake wa Wilaya au Mkurugenzi wa Halmashauri husika, Lakini kwa Jimbo la Bunda Mjini Hali ni tofauti kabisa Viongozi wote wanamahusiano mazuri na wanashirikiana katika kila jambo na ndio maana Maendeleo yanasonga mbele.

Katika tukio hili, wageni mbalimbali walihudhuria wakiwemo waheshimiwa Madiwani wakiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Mheshimiwa Michael Kweka, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda Ndg. Emmanuel Mkongo pamoja na Viongozi mbalimbali wa Chama Cha Mapinduzi.

Mbali na kugawa pikipiki Mheshimiwa Maboto amegawa pia reflector kwa madereva pikipiki wote wa Halmashauri ya Mji wa Bunda.