Mazingira FM

Bunda: Watu 13 wahofiwa kufariki dunia Ziwa Victoria

31 July 2023, 4:39 pm

Wananchi wakifuatilia zoezi la utafutaji watu 13 ambao wanahofiwa kuzama majini. Picha na Adelinus Banenwa.

Watu 13 wanahofiwa kufariki dunia huku wengine 14 wakinusurika baada ya mitumbwi miwili kuzama Ziwa Victoria wakiwa wanatoka kanisani eneo la Mchigondo kata ya Igundu halmashauri ya wilaya ya Bunda.

Na Adelinus Banenwa na Edward Lucas

Watu 13 wanahofiwa kupoteza maisha na wengine 14 wakinusurika kifo baada ya kuzama ziwa Victoria eneo la Mchigondo kata ya Igundu halmashauri ya wilaya ya Bunda mkoa wa Mara.

Kwa mujibu wa mwenyekiti wa kijiji cha Igundu, Sumila Nyamkinda Kafumu amesema tukio hilo limetokea jana tarehe 30 Julai 2023 majira ya saa 12:00 jioni wakati waumini wa Kanisa Takatifu la Mungu la Kiroho (KTMK) wakiwa wanarejea nyumbani baada ya shughuli za kanisa kijiji cha Mchigondo.

Akizungumza na Mazingira Fm, Kafumu amesema inasadikiwa walikuwa jumla ya watu 28 ambao walipanda mitumbwi miwili tofauti lakini wakiwa safarini mtumbwi wa mbele ulipata ajali na kuanza kuzama ndipo mtumbwi uliokuwa nyuma ulifika kutoa msaada lakini ulielemewa baada ya watu wengi kuuvuta kwa nyuma jambo lililopelekea mtumbwi huo pia kuzama.

Sauti ya mwenyekiti wa kijiji cha Igundu, Sumila Nyamkinda Kafumu
Mitumbwi inayotajwa kutumiwa na watu hao wakati wa safari ikiwa imetolewa na kusogezwa ufukweni katika kijiji cha Mchigondo. Picha na Adelinus Banenwa

Baadhi ya viongozi wakiongozwa na mkuu wa wilaya ya Bunda, Dr. Vicent Naano leo asubuhi wamefika katika eneo hilo na kuandelea na juhudi za utafutaji ambapo hadi kufikia mida ya mchana zoezi la utafutaji limesitishwa kutokana na hali ya hewa kuwa mbaya kutokana na upepo huku wakiweka mipango ya kuendelea na zoezi hilo hapo baadaye kwa ushirikiano wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara na wanatarajia kupata msaada zaidi kwa kikosi cha wanamaji kutoka Mwanza ili kuongeza nguvu.

Mkuu wa wilaya ya Bunda, Dr. Vicent Naano akizungumza kuhusu zoezi la utafutaji.

Kwa upande wake mkuu wa polisi kikosi cha zimamoto na uokoaji mkoa wa Mara, Augostino Magere amesema tangu walipofika eneo la tukio jitihada za kuwatafuta watu 13 wanaohofiwa kufa maji zimefanyika ambapo hadi saa saba walikuwa hawajafanikiwa kupata mtu lakini changamoto kubwa katika eneo la uokozi ni kuwa tope jingi.