Mazingira FM

Viongozi wa wajasiriamali Bunda wasimamishwa, Utata waibuka

18 July 2026, 8:07 pm

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Minza Shani Atitoa maelekezo wakati wa mkutano wa kusikiliza kero za wajasiriamali

Inadaiwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na malalamiko ya wajasiriamali pamoja na muda wa uongozi uliowekwa kwenye katiba yao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Minza Shani, amesimamisha uongozi wa Wajasiriamali Wilaya ya Bunda na kumtaka Mwenyekiti wa Wajasiriamali Mkoa wa Mara, Charles Waitara, kuhakikisha unapatikana uongozi mpya.

Na Adelinus Banenwa

Uamuzi huo umetolewa leo Julai 17, 2026, katika kikao cha wajasiriamali wa Stendi Mpya mjini Bunda, kilicholenga kusikiliza kero zinazowakabili.

Minza amesema amefikia uamuzi huo kutokana na malalamiko ya wajasiriamali pamoja na muda wa uongozi uliowekwa kwenye katiba yao.

Sauti ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Minza Shani
Baadhi ya wajasiriamali katika soko la genge la asubuhi na stendi mpya Bunda

Kwa upande wake, Charles Waitara, ambaye ni Mwenyekiti wa Wajasiriamali Mkoa wa Mara, amesema wamepokea maelekezo hayo, ingawa kuna taratibu zinazopaswa kufuatwa, ikiwemo taarifa kumfikia Mkuu wa Wilaya ya Bunda, ambaye ni mlezi wa viongozi na wajasiriamali wilayani humo.

Waitara pia ameiomba Serikali kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo, hususani katika eneo la Soko la Manjebe, ili waweze kunufaika na fursa za biashara.

Sauti ya Charles Waitara, ambaye ni Mwenyekiti wa Wajasiriamali Mkoa wa Mara
Baadhi ya wajasiriamali katika soko la genge la asubuhi na stendi mpya Bunda

Naye Diwani wa Kata ya Bunda Mjini, Elias mwita Samo, amesema aliamua kumuita Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na viongozi wengine baada ya wajasiriamali kuwasilisha kero mbalimbali, hali aliyosema imekuwa ikisababisha mgawanyiko kati ya wananchi, viongozi wa wajasiriamali na Serikali.

Awali, wajasiriamali hao walilalamikia baadhi ya viongozi kuchukua fedha bila kutoa risiti, kucheleweshwa kwa mikopo na kutozwa fedha za kujiunga kwenye masoko.