Mazingira FM

Chanzo cha maji kilichotunzwa na WWF kunufaisha wakazi 800 wa Buswahili Butiama

24 March 2024, 7:04 pm

baadhi ya viongozi wakikata utepe ishala ya uzinduzi wa chanzo cha maji cha Kyanyamatende Picha na Dinnah Shambe

Zaidi ya wananchi 800 katika kijiji cha Buswahili wilaya ya Butiama  mkoani Mara   wanufaika na chanzo cha maji cha Kyanyamatende  kilichotunzwa na kuboreshwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi na Mazingira WWF  Tanzania kwa ufadhiri wa USAID

Na Dinnah Shambe

Zaidi ya wananchi 800 katika kijiji cha Buswahili wilaya ya Butiama  mkoani Mara   wanufaika na chanzo cha maji cha Kyanyamatende  kilichotunzwa na kuboreshwa na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi na Mazingira WWF  Tanzania kwa ufadhiri wa USAID.

Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi  mradi huo kwa  wananchi ,Enock Edward ambaye ni Afisa Ufatiliaji ,Tathimini na Mafunzo WWF amesema  mradi huo ni hatua ya utekelezaji wa mpango wa Uhifadhi wa Mazingira katika Dakio la Mto Mara kwa kuhakikisha huduma ya maji yenye usalama kwa binadamu na mifugo inapatikana kwa jamii zinazoishi kandokando ya mto Mara.

Aidha Enock amesema chanzo hicho ni miongoni mwa vyanzo vya  maji vya asili vipatavyo 10 ambavyo shirika hilo limevifanyia maboresho na matunzo kupitia mradi wake wa uhifadhi wa Dakio la Mto Mara kwa ufadhili  wa shirika la misaada la watu wa marekani USAID

Amesema mradi huo wa miaka mitatu ulianza mwezi Aprili mwaka 2022 na utafikia kikomo mwaka 2025 mwezi Aprili lengo likiwa ni kuhifadhi dakio la mto Mara katika wilaya 6 na vijiji 125 vya mkoa wa Mara ambapo miongoni mwa shughuli za mradi ni kuzijengea uwezo taasisi zinazojihusisha na uhifadhi wa vyanzo vya maji, kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa jamii, kuhamasisha na kuhimiza upatikanaji wa mifumo rafiki ya uchangiaji wa shughuli za uhifadhi.

Kwa upande wa wananchi wa Buswahili wamesema maboresho yaliyofanyika yatawawezesha kupata maji kwa uhakika ambayo ni salama kwa binadamu na mifugo yao.

Naye mgeni rasmi katika hafla hiyo, Rutaremwa Rutaimirwa Katibu Tawala wilaya ya Butiama kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Butiama Mhe Mosses Kaegere amelipongeza shirika la WWF na USAID kwa juhudi za uhifadhi wa mazingira na kutoa wito kwa wananchi kulinda vyanzo hivyo vya maji kwa kuacha shughuli zote ambazo zinahatarisha uendelevu na usalama wa vyanzo vya maji.

Rutaremwa Rutaimirwa Katibu Tawala wilaya ya Butiama, Picha na Dinnah Shambe

Hafla hiyo ya kukabidhi chanzo hicho cha maji iliambatana na zoezi la upandaji wa miche ya miti zaidi ya 1000 na shughuli za usafi wa mazingira katika eneo hilo.