Mazingira FM

Bila kuwepo mahakamani, ahukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la kubaka

14 September 2023, 7:31 pm

Hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Bunda Betron Sokanya amesema  kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa na mahakama imethibitisha pasi na kuacha shaka lolote kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo

Na Adelinus Banenwa

Mahakama ya wilaya ya Bunda imemuhukumu kifungo cha miaka 30 jela Dancan Vicent kwa kosa la kubaka kinyume na kifungu cha 130 (1) na (2) (e) nakifungu cha 131(1) cha  sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Akisoma hukumu hiyo hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya wilaya ya Bunda Betron Sokanya amesema  kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa na mahakama imethibitisha pasi na kuacha shaka lolote kuwa mtuhumiwa alitenda kosa hilo

Awali ilielezwa na mwendesha mashtaka wa mahakama hiyo  Athumani  Salimu kuwa mshtajiwa alitenda kosa hilo la kumbaka binti mwenye umri wa miaka 15 ambaye alikuwa muhitimu wa darasa la saba katika shule ya msingi namibu tarehe 12/06/2022 majira ya jioni huko katika kijiji cha Namibu (w) Bunda na mshtajiwa kutorokea pasipofahamika mpaka alikamatwa mwezi wa 12 /2022.

Mwendesha mashtaka aliiomba mahakama itoe adhabu kali ili iwe fundisho kwa mshtakiwa na jamii ijfunze kuacha tabia kama za mshtakiwa na matokeo yake jamii isaidie watoto wa kike kufikia ndoto zao.

Hukumu hii imesomea bila uwepo wa mshtakiwa ambapo alitoroka baada ya kukamatwa mara ya kwanza kisha kupewa dhamana kwa mujibu wa sheria  huku mahakama ikielekeza  kuwa adhabu hii itaanza kutumika mara mshtakiwa atakapokamatwa tena na jeshi la polisi linaendelea kumsakanya mshtakiwa huyo.