Mazingira FM

Utafutaji watu 13 waliozama Ziwa Victoria waendelea leo bila mafanikio

31 July 2023, 10:44 pm

Baadhi ya wananchi waliokusanyika kando ya ziwa Victoria eneo la Mchigondo kwa ajili ya zoezi la utafutaji wanaohofiwa kufa maji. Picha na Adelinus Banenwa

Hakuna hata mmoja aliyepatikana hadi kufikia jioni ya leo 31 July 2023 kati ya 13 wanaohofiwa kufa maji eneo la Mchigondo Wilaya ya Bunda baada ya mitumbwi miwili kuzama Ziwa Victoria jana 30 July 2023 majira ya saa 12:30 jioni

Na Adelinus Banenwa na Edward Lucas

Zoezi la utafutaji watu 13 wanaoshukiwa kufa maji Ziwa Victoria katika kijiji cha Mchigondo limeendelea tena leo pasipo mafanikio.
Katika zoezi hilo lililoanza tangu jana 30 July 2023 majira ya saa 12:30 lilipotokea tukio hilo, limeendelea tena leo kwa ushirikiano wa wananchi na kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara ambapo hadi jioni ya leo 31 July 2023 hakuna hata mtu mmoja aliyepatikana.
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara, Augosto Magere ameeleza changamoto wanazokutana nazo katika zoezi hilo ni pamoja na hali ya hewa, kiza kinene na wingi wa tope.

Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mara, Augosto Magere

Tukio hilo la watu kuzama kwenye maji limetokea katika kijiji cha Mchigondo kata ya Igundu Halmashauri ya Wilaya wa Bunda wakati waumini wa Kanisa Takatifu la Mungu la Kiroho KTMK wapatao 28 walilopanda kwenye mitumbwi miwili tofauti kisha kuzama huku watu 14 kunusurika, mtoto mmoja akifariki dunia na wengine 13 hawajulikani walipo.