Mazingira FM

UWT BUNDA; Waadhimisha miaka 46 ya CCM kwa kuchangia fedha na saruji shule ya msingi Kabarimu.

25 January 2023, 8:29 am

Jumuiya ya wanawake chama cha mapinduzi wilaya ya Bunda UWT imechangia kiasi cha shilingi laki saba na mifuko hamsini ya saruji shule ya msingi Kabarimu ili kupunguza adha wanayoipata wanafunzi wa shuleni hapo wanaokaa  chini kwenye vumbi wakati wa kusoma.

Fedha na saruji hizo zimetolewa ikiwa ni maadhimisho ya  miaka 46 ya kuzaliwa chama cha mapinduzi CCM ngazi ya wilaya kwa jumuiya hiyo ambapo mgeni rasmi alikuwa ni Mwenyekiti wa UWT mkoa wa Mara NANCY SESAN

Katibu wa jumuiya ya wanawake wilaya ya Bunda Evodia Zumba amesema wameamua kufanya maadhimisho hayo katika shule ya msingi Kabarimu kutokanana changamoto ya upungufu wa madawati, na kuwepo kwa madarasa ambayo hayana sakafu hivyo wanafunzi wengi kukaa chini kwenye vumbi.

Evodia ameongeza kuwa hali hiyo ilibainika katika ziara ya kamati ya siasa ya chama hicho wakati wa ukaguzi wa utekelezaji wa ilani ya chama hicho ambapo katika shule ya msingi Kabarimu ‘A’ walikuta darasa la kwanza hadi darasa la nne wanakaa kwenye madarasa ambayo hayana sakafu wala madawati jambo linalowafanya watoto hao kukaa chini kwenye vumbi.

Kwa upande wake mgeni rasmi  katika maadhimisho hayo amewatolea wito viongozi wilayani Bunda kuona umuhimu wa shule hiyo ya kabarimu kwa kuwa na miundombinu rafiki kwa watoto huku akihaidi kuwaleta viongozi wengine wa kitaifa katika shule hiyo ambayo kwa mujibu wa taarifa ya mwalimu mkuu alianzishwa mwaka 1974 kabla ya mwaka 2006 kuigawa kuwa shule mbili yaani kabarimu ‘A’ na’ B’

Awali akisoma taarifa kwa mgeni rasmi mwalimu mkuu wa shule ya msingi kabarimu a amesema jumla ya vyumba vya madarasa 10 havina sakafu kabisa hivyo  kupelekea watoto wanaosomea kwenye madarasa hayo kuakaa chini kwenye vumbi