Mazingira FM

Bunda: Mamba wanatumaliza kwa kuwa hatuna maji ya bomba

17 February 2024, 9:52 pm

Ukosefu wa huduma ya maji ya bomba yatajwa kuwa chanzo cha wananchi kushambuliwa na mamba Halmashauri ya wilaya ya Bunda.

Na Adelinus Banenwa

Ukosefu wa huduma ya maji ya bomba yatajwa kuwa chanzo cha wananchi kushambuliwa na mamba Halmashauri ya wilaya ya Bunda.

Hayo yameelezwa  katika kikao cha baraza la madiwani robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023 na 2024 kilichoketi 16 Feb 2024.

Katika kikao hicho madiwani wamesema changamoto kubwa ni kwa kata zinazozunguka ziwa Victoria ndani ya halmashauri ya wilaya ya Bunda.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Bunda Mhe Charles Magafu Manumbu, Picha na Adelinus Banenwa

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Mhe Charles Magafu Manumbu  amesema ili kunusuru maisha ya wananchi   serikali haina budi kupeleka huduma ya maji kwa wananchi.

Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda Bi Changwa Mkwazu, Picha na Adelinus Banenwa

Naye Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Bunda Bi Changwa Mkwazu  amesema kutokana na changamoto kubwa ya mamba tayari halmashauri ya wilaya kwa kushirikiana na ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bunda wamezungumza na mamlaka ya wanyamapori TAWA namna ya kupunguza athari za Mamba hao.

katibu tawala wilaya ya Bunda Salumu Mtelela, Picha na Adelinus Banenwa

Naye katibu tawala wilaya ya Bunda Salumu Mtelela amewataka madiwani ambao kata zao zinapakana na ziwa Victoria kutoa elimu  kwa wananchi kuchukua tahadhari ya mamba kama wataalamu wanavyo elekeza kama vile kuepuka  kwenda kuoga ndani ya ziwa, kuepuka kufua ndani ya ziwa pamoja na shughuli zingine zenye hatari.

Aidha katibu tawala amewahakikishia madiwani kuwa pamoja na changamoto za mamba serikali inachukua hatua ikiwa ni pamoja na kushirikiana na TAWA pamoja na mamlaka za maji  ikiwa ni pamoja na BUWASA na RUWASA ili kufikisha maji kwa wananchi .

Mmoja ya wananchi akiosha vyombo kando ya ziwa sehemu inayotajwa kuwa na mamba, Picha na Adelinus Banenwa

Radio Mazingira Fm ilishuhudia hali ya wakazi wa moja ya kijiji ndani ya halmashauri ya wilaya ya Bunda wanaotumia maji ya ziwa hilo kuoga na kufulia wakidai hawana namna kutokana na kukosa huduma ya maji ya bomba wanalazimika kufulia ziwani.