Mazingira FM

Jukwaa la wadau wa kilimo Bunda, larasimishwa rasmi

13 December 2023, 9:32 am

Baraka Kamese kutoka BUFADESO. picha na Thomas Masalu

Jukwaa la wadau wa kilimo wilaya Bunda linalokutanisha halmashauri ya Bunda mji na Bunda Dc limerasimishwa rasmi kupitia kikao kilichofanyika Dec 8 mwaka 2023 katika ukumbi wa Shaloom mjini Bunda.

Na Thomas Masalu

Jukwaa la wadau wa kilimo wilaya Bunda linalokutanisha halmashauri ya Bunda mji na Bunda Dc limerasimishwa rasmi kupitia kikao kilichofanyika Dec 8 mwaka 2023 katika ukumbi wa Shaloom mjini Bunda.

Jukwaa hilo litafanya kazi zake kupitia Uchechemuzi wa masuala ya kilimo katika sera, sheria, kanuni na miongozo ili kuweza kusaidia mkulima kunufaika na kilimo chake.

Akitoa taarifa ya umuhimu wa jukwaa hilo mwenyekiti wa jukwaa hilo Mashaka Paul amesema jukumu lao kubwa ni kufanya uchechemuzi katika sera za kilimo, sheria, kanuni na miongozo ili kuweza kusaidia mkulima kunufaika na kilimo chake hasa wale wakulima wadogo.

‘Jukwaa hili lina umuhimu mkubwa mno, hasa katika kuchechemua sera za kilimo, sheria, kanuni na miongozo, lengo ni kuwafikia watoa maamuzi’ amesema Paul Mashaka Mwenyekiti wa Jukwaa

Nyagera Runkiko Mkulima kiongozi mkazi wa Kunzugu amesema wakulima wadogo wamepata chombo chao cha kwa kuwaunganisha na watunga sera pamoja na watoa maamuzi lengo kubwa likiwa ni utatuzi wa changamoto za wakulima wadogo ambao wamekuwa wakilalamika muda mrefu.

‘ Hiki ni chombo chao wakulima wadogo, hata mimi nimefurahi sana kuwa sehemu ya jukwaa hili, wakulima wadogo tumelia mno muda mrefu lakini kupitia jukwaa hili naimani linaenda kutuunganisha na watunga sera na watoa majibu’ amesema Mkulima kiongozi Nyagera Runkiko

Kwa upande wake mratibu wa shirika la Bunda Farmers Development Support Organization (BUFADESO) Baraka Kamese amesema wao ndio wenye jukumu la kulea jukwaa hilo hivyo watahakikisha wana waunganisha na watunga sera na watoa maaamuzi ili malengo ya jukwaa yatimie.

‘ Sisi BUFADESO jukumu letu ni kulea jukwaa hili, kwahiyo sisi tutahakikisha tunapambana kwenye vikao hivi tunawaleta watunga sera na watoa maamuzi ili changamoto za wakulima wadogo zipate ufumbuzi’ amesema Baraka Kamese Mratibu wa shirika la Bufadeso

Nemence Iriya ni mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali Civic social protection foundation (CSP)amesema uwepo wa majukwaa ya kilimo kutasaidia kubeba ajenda mbalimbali za wakulima katika kilimo endelevu chenye kuboresha Maisha, kuimarisha taasisi za kilimo na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

‘Uwepo wa majukwaa haya yatasaidia sana kubeba ajenda za wakulima wadogo’ amesema Nemence Iriya ni mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali Civic social protection foundation (CSP)

Hata hivyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Michael Thomas Kweka ambaye ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika shughuli hiyo amesema wataendelea kutoa msukumo kwa serikali kupitia vikao vya halmashauri ili wakulima wadogo wanufaike na jasho lako.

‘Tutaendelea kutoa msukumo kwa serikali kupitia vikao vyetu vya halmashauri ili wakulima wadogo wanufaike na jasho lako’ amesema Kweka mwenyekiti wa halmashauri ya mji wa Bunda

Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1997 na marekebisho yake (URT, 1977; URT, 2009), ambayo iliweka serikali za mitaa kuhakikisha ushiriki wa raia katika maamuzi ya sera na bajeti.
Kupitia ibara ya 145 (1) na 146 (1) ya katiba inayosema

“Kutakuwa na vyombo vya Serikali za Mitaa katika kila mkoa, wilaya, mji na kijiji, katika Jamhuri ya Muungano,ambavyo vitakuwa vya aina na majina yatakayowekwa na sheria iliyotungwa na Bunge au na Baraza la Wawakilishi.” na

“Madhumuni ya kuwapo Serikali ya Mitaa ni kupeleka madaraka kwa wananchi. Na vyombo vya Serikali za Mitaa vitakuwa na haki na mamlaka ya kushiriki kuwashirikisha wananchi katika mipango na shughuli za utekelezaji wa maendeleo katika sehemu zao na nchini kote kwa jumla”

Wazo la uundaji wa majukwaa umetokana na mradi wa ASILI-B unaotekekezwa katika halmashauri tano kwa mkoa wa Mara ambapo halmashauri ya mji wa Bunda na halmashauri ya wilaya ya Bunda ni wanufaika wa mradi huo.