Mazingira FM

Mtanda awapongeza WWF kwa uhifadhi Mto Mara

13 September 2023, 6:05 pm

Mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda akiendesha zoezi la upandaji miti na uwekaji wa bikoni kando ya bonde la Mto Mara

Na Edward Lucas

Mkuu wa mkoa wa Mara, Said Mtanda amelipongeza Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira WWF na wadau wengine katika juhudi wanazozifanya katika kuulinda Mto Mara

Mtanda ametoa kauli hiyo leo wakati wa zoezi la upandaji wa miti na uwekaji wa bikoni au vigingi kandokando ya mto Mara katika kijiji cha Borenga Wilaya ya Serengeti katika kuadhimisha siku ya Mto Mara.

Sauti ya Mhe. Mtanda akiwapongeza WWF na wadau wengine kwa Uhifadhi wa mto Mara

Katika zoezi hilo linalotekelezwa maeneo mbalimbali kwenye mkondo wa bonde la Mto Mara, WWF kwa ufadhili wa USAID wamekusudia kupanda miche 44,000 na kuweka vigingi 50 ili kuweka alama zitakazosaidia wananchi kutofanya shughuli zao ndani ya mita 60 katika bonde la mto.

Awali akisoma taarifa fupi ya Uhifadhi wa bonde la Mto Mara, Afisa Mazingira Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Helga Enock Nkongoki amesema jumla ya miti 5000 imeshapandwa eneo la la Nyasurura na Marenge huku miche 500 iliyotolewa na WWF ikipandwa leo eneo la Borenga Serengeti.

Helga Enock Nkongoki akisoma risala ya utekelezaji wa zoezi la upandaji wa miti na uwekaji wa bikoni
Viongozi na wananchi wakishiriki zoezi la upandaji wa miti 500 eneo la cha Borenga Wilaya ya Serengeti