Mazingira FM

Upatikanaji wa pembejeo ni changamoto kwa wakulima wadogo

13 December 2023, 9:17 am

Baraka Kamese ni mratibu wa shirika la BUFADESO. Picha na Thomas Masalu

Utafiti mdogo uliofanywa na Shirika la Civil Social Protection Foundation (CSP) kwa kushirikiana na shirika la MVIWANYA umebaini kuwa upatikanaji wa pembejeo ni changamoto kwa wakulima wadogo.

Na Thomas Masalu

Utafiti mdogo uliofanywa na Shirika la Civil Social Protection Foundation (CSP) kwa kushirikiana na shirika la MVIWANYA umebaini kuwa upatikanaji wa pembejeo ni changamoto kwa wakulima wadogo.

Utafiti huo unaoitwa ‘Utafiti kuhusu masuala muhimu ya kisera, kimfumo na kiprogramu yanayowakabili wakulima wadogo’ wa mwaka 2023 ulihusisha wakulima wadogo 72 katika mikoa ya Kagera na Mara.

Matokeo ya utafiti huo yanaonyesha asilimia 36 ndio wamewahi kupokea pembejeo kama vile mbegu, dawa na mbolea katika kipindi cha miaka mitatu huku asilimia 75% wameonyesha kuwa na taarifa ya Serikali kwamba inatoa pembejeo kwa wakulima.

‘Asilimia 39% wamethibitisha kuwa pembejeo zilisafirishwa hadi kijijini wanamoishi huku asilimia 61% wamesema wamekuwa wakisafiri hadi kilomita 50 na kutumia zaidi ya TZS 40,000 kwa kufuata pembejeo hizo katika ofisi za kata, ofisi za wilaya, maduka ya pembejeo mjini na katika ofisi za mikoa’ inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Pia ripoti hiyo imesema asilimia 1% ya wakulima wamethibitisha kuwa pembejeo zilifika kwa wakati katika eneo lao.

Silas Yona mkazi wa Kunzugu amesema Serikali iweke mipango mathubuti ya kupeleka pembejeo kwa wakulima ikiwa ni Pamoja na kuongeza bajeti ya kupeleka pembejeo hizo ili zifike kwa wakati na karibu.

‘Kwa mfano mimi nizungumzie zao la pamba, ukiangalia wakulima wakubwa hawatumii pembejeo kutoka bodi ya pamba maana yake bila kutumia pesa yako matokeo yanakuwa hakuna’ amesema Mkulima Silas Yona mkazi wa Kunzugu

‘Mwisho wa unyunyuziaji dawa ndio zinakuja kwa wingi wakati zinakuwa hazina tija wakati wakunyunyuzia dawa hawaleti’ ameongezea

Mariam Marwa mkulima mkazi wa sazira amesema viongozi wawatembelee wakulima wadogo katika vijiji vyao ili kujua namna wakulima wanavyoendelea na kuwaeleza juu ya upatikanaji wa pembejeo na masoko.

‘Sasa nikwambie mwandishi unajua tupo tupo tu, hatuoni kiongozi akija atuambie madawa yanapatikana wapi, sasa tunajilimia tu’ amesema Mariam Marwa mkazi wa Sazira

Kwa Upande wake Nyagera Runkiko ambaye ni mkulima kiongozi amesema kuna changamoto katika ugawaji pale anapowaalika wakulima kwenda kuchukua pembejeo wanaenda na ambao si wakulima mwisho wa siku zinapelea kukidhi mahitaji ya wakulima.

Baraka Kamese ni mratibu wa shirika la BUFADESO amesema pembejeo za kilimo ambazo ni pamoja na mbegu bora, mbolea na viuatilifu za kulinda mazao dhidi ya wadudu waharibifu, ni muhimu kwa mafanikio ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.

‘Unapowezesha wakulima wadogo kwa kuwapatia mbegu bora, mbolea na viuatilifu vya kulinda mazao dhidi ya wadudu waharibifu kwa wakati, utakuwa umefanya jambo kubwa mno’ amesema Baraka Kamese

Hata hivyo Sera ya Taifa ya Kilimo ya mwaka 2013, kifungu cha 3.9.3 (i) kinasema, “Serikali itatekeleza sheria na sera ili kuwalinda wakulima dhidi ya usambazaji wa pembejeo zisizokidhi viwango”

Na kifungu cha 3.9.3 (v) ambacho kinachosema “Wakulima watasaidiwa kupata pembejeo za kisasa”