Mazingira FM

Nyatwali: Miti yakatwa, nyaraka za tathmini ya fidia zachukuliwa mikopo kisa ugumu wa maisha

14 July 2023, 1:04 pm

Baadhi ya miti iliyokatwa na wananchi wa Nyatwali kwa lengo la kuchoma mkaa ili wajikimu kimaisha, Picha na Edward Lucas

Baadhi ya wakaazi wa Nyatwali waanza kutumia nyaraka zao za tathmini ya fidia kuchukulia mikopo kwa ahadi ya kurejesha watakapolipwa huku wengine wakikata miti kwa ajili ya mkaa na kuuza ikielezwa ni kutokana na ugumu wa maisha.

Na Edward Lucas

Ikiwa serikali bado inaendelea na mchakato wa kuwahamisha wakaazi wa  kata ya Nyatwali Halmashauri ya Mji wa Bunda, mapya yaibuka kwa wananchi kuanza kukata miti kwa ajili ya kuuza na kuchoma mkaa na kujitumbukiza kwenye mikopo kwa dhamana za nyaraka za fidia na tathimini ili kujikimu kimaisha.

kukosa uhakika wa chakula na makazi bora hivyo kujikuta wanaingia katika mikopo-umiza kwa kuweka dhamana nyaraka zao za fidia

Hayo yamebainika jana tarehe 13 July 2023 kupitia mahojiano ya Mazingira Fm na wananchi wa maeneo hayo mtaa wa Kariakoo wakati ilipowatembelea kwa lengo la kujua nini zaidi kinachoendelea katika zoezi la kuhamishwa.

Baadhi ya miti iliyokatwa na wananchi wa Nyatwali kwa lengo la kuchoma mkaa ili wajikimu kimaisha, Picha na Edward Lucas

Wamesema tangu ulipoanza mchakato wa kuhamishwa walielekezwa kutoendeleza makazi wala kulima mazao ya muda mrefu jambo ambalo limepelekea baadhi kukosa uhakika wa chakula na makazi bora hivyo kujikuta wanaingia katika mikopo-umiza kwa kuweka dhamana nyaraka zao za fidia kwamba watarejesha baada ya kuwa wamelipwa fidia.

Hali hiyo imethibitishwa na Diwani wa Kata hiyo, Malongo Mashimo alipotafutwa na Mazingira Fm kwa njia ya simu na kusema kuwa kufuatia hali hiyo ameomba serikali iwasaidie wananchi kupata huduma ya mahindi ya bei nafuu na iharakishe mchakato kwani wameshindwa kujishughulisha na uzalishaji mali na shughuli zingine za maendeleo.

Malongo Mashimo Diwani wa Kata ya Nyatwali

Aidha katika hatua nyingine baadhi ya wananchi waliotathiminiwa maeneo yao yalioingia ndani ya maji maarufu kama ‘masanga’ wameishukuru serikali kwa kusikia kilio chao huku wale waliokosa nafasi hiyo kwa kigezo cha kukosa hati za maeneo yao wakiiomba serikali iangalie namna ya kuwasaidia kutokana na kuwepo kwa changamoto mbalimbali zilizokwamisha kupata hati hizo.

Mkazi wa kata ya Nyatwali