Mazingira FM

HOPE FOR GIRLS yasisitiza msaada wa kisaikolojia kwa manusura wa ukatili wa kijinsia

18 July 2026, 8:50 pm

kituo cha Hope for Girls and Women in Tanzania

Shirika hilo limehudumia takribani watoto 4,578 kwa kuwapatia hifadhi ya muda, msaada wa kisaikolojia, ushauri nasaha, fursa ya kuendelea na elimu pamoja na huduma nyingine

Na Edward Lucas

Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samweli, amesema msaada wa kisaikolojia ni sehemu muhimu ya kuwasaidia watoto walionusurika ukeketaji, ndoa za utotoni na aina nyingine za ukatili wa kijinsia kurejesha matumaini na kuendelea na maisha yao.

sauti ya Rhobi Samweli
Mkurugenzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samweli

Akizungumza na Radio Mazingira Fm, Rhobi amesema kupitia Nyumba Salama, watoto hupatiwa ushauri nasaha kwa njia ya mazungumzo ya mtu mmoja mmoja na ya makundi kwa kushirikiana na wataalamu wa ustawi wa jamii, dawati la jinsia na wadau wengine. Amesema hatua hiyo huwasaidia kuwajengea hali ya kujiamini, kubaini changamoto zilizojificha na kupanga huduma zinazokidhi mahitaji ya kila mtoto.

sauti ya Rhobi Samweli

Kwa upande wake, Matroni wa Nyumba Salama, Terecia Pius, amesema watoto wanaowasili kituoni hupokewa kwa upendo na kushirikishwa katika shughuli mbalimbali ikiwemo elimu, michezo, malezi ya kiimani na ukuzaji wa vipaji, hatua ambazo zimekuwa zikiwasaidia kuondokana na hofu na kurejesha hali yao ya kisaikolojia.

sauti ya Terecia Pius

Miongoni mwa watoto wanaolelewa katika kituo hicho wamesema baada ya kunusurika ukeketaji na kupokelewa katika Nyumba Salama, wameweza kuendelea na masomo na sasa wana matumaini ya kutimiza ndoto zao, tofauti na maisha waliyokuwa wakiishi kabla ya kufika kituoni.

sauti za manusura

Hope for Girls and Women in Tanzania ni shirika lililoanzishwa mwaka 2017 lenye makao makuu Wilaya ya Serengeti, Mkoa wa Mara, likiwa na lengo la kupambana na ukatili wa kijinsia hususan ukeketaji na ndoa za utotoni. Kupitia vituo viwili vya Nyumba Salama vilivyopo Serengeti na Butiama, shirika hilo limehudumia takribani watoto 4,578 kwa kuwapatia hifadhi ya muda, msaada wa kisaikolojia, ushauri nasaha, fursa ya kuendelea na elimu pamoja na huduma nyingine za kuwawezesha kujenga maisha yao ya baadaye.