Mazingira FM
Mazingira FM
15 May 2026, 11:11 am

Kuchukua dawa za VVU si jambo la aibu bali ni hatua muhimu ya kulinda afya na kuongeza ubora wa maisha kwa waathirika.
Na Thomas Masalu
Diwani wa Kata ya Bunda Stoo Flavian Chacha amehoji kuhusu utaratibu wa uchukuaji wa dawa za VVU katika vituo vya kutolea huduma za afya, akitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa kuhakikisha faragha ya wahitaji inalindwa pamoja na namna watoto wanaweza kuzuiwa kuambukizwa VVU kutoka kwa mama zao.

Swali hilo limeibuliwa kufuatia kuwepo kwa mtazamo hasi katika jamii ambapo baadhi ya watu bado huona aibu kwenda kuchukua dawa za VVU katika maeneo ya wazi kama zahanati, hospitali na vituo vya afya kwa hofu ya kunyanyapaliwa au kuhukumiwa na jamii.
Akijibu swali hilo, mganga mkuu wa halmashauri ya mji wa bunda daktari Yusuph Wambura amesema kuchukua dawa za VVU si jambo la aibu bali ni hatua muhimu ya kulinda afya na kuongeza ubora wa maisha kwa waathirika.
Ameeleza kuwa vituo vya afya vinaendelea kuboresha mifumo ya utoaji huduma ili kuhakikisha siri za wagonjwa zinalindwa na kila mhitaji anapata huduma kwa heshima na usiri unaostahili.
Kuhusu namna mtoto anavyoweza kukingwa dhidi ya maambukizi kutoka kwa mama mzazi, daktari Wambura amefafanua kuwa mama mjamzito mwenye maambukizi ya VVU anapaswa kuwahi kliniki, kufuata ushauri wa wataalamu wa afya na kutumia dawa za kufubaza virusi kwa usahihi katika kipindi chote cha ujauzito na baada ya kujifungua.
Ameongeza kuwa mtoto pia hupewa kinga maalum mara baada ya kuzaliwa na kufuatiliwa kiafya kwa karibu, hatua ambazo husaidia kwa kiwango kikubwa kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.