Mazingira FM
Mazingira FM
9 July 2026, 11:44 am

Dhana ya “Kupinga ukatili wa Kijinsia mahali ulipo” inatokana na ukweli kwamba vitendo vya ukatili hufanyika ndani ya familia na jamii tunazoishi nazo kila siku.
Na Edward Lucas
Mwenyekiti wa Jukwaa la Kupinga Ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Mara (LeMaChU), Penina Jonathan Daud, amesema mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yatafanikiwa endapo kila mwananchi atachukua jukumu la kupinga vitendo hivyo mahali alipo.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mazingira Fm, Penina amesema dhana ya “Kupinga ukatili wa Kijinsia mahali ulipo” inatokana na ukweli kwamba vitendo vya ukatili hufanyika ndani ya familia na jamii tunazoishi nazo kila siku, hivyo kila mmoja ana nafasi ya kuzuia na kuripoti ukatili kabla haujaleta madhara makubwa.
Amesema pamoja na kuendelea kutolewa kwa elimu ambayo imechangia kupungua kwa baadhi ya matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Mara, bado vitendo hivyo vinaendelea kujitokeza.
Ametaja mauaji ya wanandoa, mimba na ndoa za utotoni pamoja na ukeketaji kuwa miongoni mwa changamoto zinazoendelea kuathiri wanawake na watoto.
Kwa mujibu wa Penina, moja ya sababu zinazokwamisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia ni wananchi wengi kushindwa kutoa taarifa wanaposhuhudia au kufahamu matukio ya ukatili, hali inayowapa nafasi wahusika kuendelea kufanya vitendo hivyo bila kuchukuliwa hatua.
Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kuendelea kushirikiana, kutoa taarifa za matukio ya ukatili kwa mamlaka husika na kuendeleza elimu katika jamii, akisisitiza kuwa kaulimbiu ya “Mara Bila Ukatili wa Kijinsia Inawezekana” inaweza kutimia ikiwa kila mmoja atatimiza wajibu wake wa kulinda haki na usalama wa wanawake na watoto.