Mazingira FM
Mazingira FM
19 August 2026, 11:46 am

Kwa baadhi ya jamii mkoani Mara, miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba hutajwa kuwa kipindi cha hatari, ambapo vitendo vya ukeketaji huongezeka.
Na Edward Lucas
Wadau wa kupambana na ukatili wa kijinsia mkoani Mara wametaka mikakati ya kuzuia ukeketaji kuanza kabla ya msimu wa vitendo hivyo, huku wakisisitiza umuhimu wa kuwashirikisha mangariba na kuwatafutia njia mbadala za kujipatia kipato.
Kwa baadhi ya jamii mkoani Mara, miezi ya Oktoba, Novemba na Desemba hutajwa kuwa kipindi cha hatari, ambapo vitendo vya ukeketaji huongezeka, hasa wakati wa likizo za wanafunzi.
Aliyewahi kuwa ngariba kwa muda mrefu na ambaye ameacha shughuli hiyo, Rhobi John, amesema kipindi hicho huwaweka watoto wa kike katika mazingira hatarishi, huku baadhi yao wakikabiliwa na ugumu wa kutoroka kutokana na ulinzi na usimamizi unaowekwa na familia.
Rhobi John amesema katika kutafuta suluhisho la kudumu, jamii inapaswa kuangalia pia changamoto za kiuchumi zinazowafanya baadhi ya mangariba kuendelea na shughuli hiyo.
Amesema kukaa nao, kuzungumza nao na kuwapatia fursa mbadala za kiuchumi kunaweza kusaidia kupunguza utegemezi wao katika ukeketaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania, Rhobi Samwelly, amesema changamoto hiyo inaonekana pia katika ongezeko la watoto wanaofika Nyumba Salama wakikimbia ukeketaji.
Amesema msimu uliopita kituo hicho kilipokea watoto wapya zaidi ya 250, licha ya bajeti kuandaliwa kwa ajili ya watoto 100, hali iliyoongeza mahitaji ya chakula, matibabu, mavazi na mahitaji mengine ya msingi.
Amesema shirika hilo limeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji na kushirikiana na baadhi ya watu waliowahi kujihusisha na vitendo hivyo, kwa lengo la kupata suluhisho la kudumu.
Wakati Oktoba hadi Desemba 2026 ikitajwa kuwa kipindi cha hatari katika baadhi ya jamii, wadau wamesisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukeketaji hayawezi kutegemea watoto kukimbia pekee, bali yanahitaji elimu ya mapema, ulinzi wa watoto, ushiriki wa familia na jamii, pamoja na kuwapatia waliowahi kujihusisha na vitendo hivyo njia salama za kujipatia kipato.