Mazingira FM
Mazingira FM
19 August 2026, 6:22 pm

Miongoni mwa kero zilizowasilishwa ni zoezi la ugawaji wa vyandarua vilivyotolewa na Serikali.
Na Juma Hangi
Wakazi wa Mtaa wa Saranga wamewasilisha kero mbalimbali zinazowakabili katika kikao kilichofanyika Agosti 18, 2026, kilichoitishwa na Mwenyekiti wa Mtaa huo, Philipo Safari, kwa lengo la kujadili changamoto za wananchi na kutafuta ufumbuzi. Kikao hicho kilihudhuriwa na Diwani wa Kata ya Kabarimu, Kulwa Ramadhan Ngata, pamoja na Mtendaji wa Kata hiyo, ambapo wananchi walipata fursa ya kueleza kero zao moja kwa moja kwa viongozi.
Miongoni mwa kero zilizowasilishwa ni zoezi la ugawaji wa vyandarua vilivyotolewa na Serikali, ambapo wananchi wamedai kuwa zoezi hilo halikufanyika kwa usawa na haki. Baadhi yao wamedai kuwa kulikuwa na utofauti wa idadi ya vyandarua walivyopatiwa wananchi, huku wakitaka viongozi kufuatilia utaratibu uliotumika katika ugawaji huo na kuhakikisha wananchi wote wenye uhitaji wanapata huduma hiyo kwa usawa.

Kwa upande wake mwenyekiti wa mtaa wa Saranga Philipo Safari amesema kuwa madai ya ugawaji vyandarua usiokuwa na haki na usawa wameipokea ofisini na wataifanyia kazi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kabarimu, Kulwa Ramadhan Ngata, amesema amelichukua suala la ugawaji wa vyandarua na analifanyia kazi, huku akichukua orodha ya majina ya wananchi ambao hawajapata vyandarua ili kufuatilia suala hilo. Aidha, amewataka wananchi wenye migogoro ya ardhi kusubiri majibu ya hatua zinazochukuliwa, ambayo amesema yatatolewa Ijumaa, Agosti 21, 2026.