Mazingira FM

Afisa uvuvi Bunda DC: Uvuvi haramu chanzo upungufu wa samaki

16 May 2026, 11:03 am

Afisa Uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, kutoka wizara ya uvuvi Raulent Nguziro

Baadhi ya wavuvi wamekuwa wakitumia nyavu za dagaa kuvulia samaki, hali inayochangia kuvuliwa kwa samaki wakiwa bado wadogo na hivyo kuhatarisha ongezeko la samaki katika Ziwa Victoria.

Na Mariam Mramba

Afisa Uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, kutoka wizara ya uvuvi Raulent Nguziro, amewaomba madiwani kushirikiana kwa karibu katika kuimarisha sekta ya uvuvi ili kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo, ikiwemo uvuvi usiofaa na kukomesha uvuvi haramu.

Rai hiyo ameitoa Mei 15, 2026 kupitia kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kilichofanyika katika ukumbi wa halmashauri hiyo.

Nguziro amesema baadhi ya wavuvi wamekuwa wakitumia nyavu za dagaa kuvulia samaki, hali inayochangia kuvuliwa kwa samaki wakiwa bado wadogo na hivyo kuhatarisha ongezeko la samaki katika Ziwa Victoria.

Aidha, amesema hali ya uzalishaji katika sekta ya uvuvi imeendelea kushuka siku hadi siku kutokana na vitendo vya uvuvi visivyozingatia sheria na kanuni za uvuvi endelevu.

Pia ameeleza kuwa baadhi ya wavuvi wa dagaa wamekuwa hawazingatii muda wa kufunga shughuli za uvuvi wakati wa giza, jambo linalosababisha kuvuliwa kwa dagaa wadogo na kuathiri ukuaji wa rasilimali za maji.

Sauti ya Afisa Uvuvi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, kutoka wizara ya uvuvi Raulent Nguziro

Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya madiwani, viongozi wa vijiji na wananchi katika kutoa elimu na kusimamia sheria za uvuvi ili kulinda rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.