Mazingira FM
Mazingira FM
12 June 2026, 3:07 pm

Ukatili wanaopitia wazee ni pamoja an kutelekezwa na wakati mwingine kuachiwa jukumu la kulea wajukuu bila msaada wa kutosha.
Na Adelinus Banenwa
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Waryoba Juma Waryoba, amesema kuwa wazee bado wanakabiliwa na vitendo mbalimbali vya ukatili katika jamii.
Akizungumza kupitia Mazingira FM, Waryoba amesema vitendo hivyo ni pamoja na kutelekezwa na wakati mwingine kuachiwa jukumu la kulea wajukuu bila msaada wa kutosha. Aidha, baadhi ya wazee hukumbwa na ukatili wa kisaikolojia unaojumuisha kutukanwa na kunyimwa chakula.
Ameongeza kuwa wazee wengine hukumbwa na ukatili wa kiuchumi unaohusisha kutapeliwa, kuibiwa na kudhulumiwa mali zao, huku wengine wakifanyiwa ukatili wa kimwili ikiwemo kupigwa.
Ametoa rai kwa jamii kuhakikisha wazee wanaheshimiwa, wanalindwa na wanapatiwa haki zao za msingi ili kuondokana na vitendo vya ukatili vinavyoathiri ustawi wao.
Waryoba ameyasema hayo wakati akizungumza kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee, ambayo huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Juni kwa lengo la kuhamasisha jamii kulinda haki na ustawi wa wazee pamoja na kupinga aina zote za ukatili dhidi yao.