Mazingira FM
Mazingira FM
24 July 2026, 9:42 pm

Maboresho hayo yataongeza ufanisi wa ufundishaji kwa vitendo kwa kuwa wanafunzi wataweza kutumia vifaa vya maabara kwa urahisi zaidi.
Na Edward Lucas
Changamoto ya ukosefu wa huduma ya maji iliyokuwa ikiathiri matumizi ya maabara mpya ya Fizikia katika Shule ya Sekondari Rubana, imeanza kupata suluhisho baada ya shule hiyo kupata tanki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 5,000 pamoja na maboresho ya mfumo wa maji, gesi na umeme katika jengo hilo.
Maboresho hayo yanatarajiwa kuongeza ufanisi wa masomo ya vitendo kwa wanafunzi 787 wa shule hiyo ambao kwa muda walikabiliwa na changamoto ya kukosa baadhi ya huduma muhimu katika maabara.
Akizungumza baada ya kukabidhi tanki hilo, Katibu wa Ofisi ya Mbunge wa Bunda Mjini, Mussa Hussein, amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika uwepo wa changamoto ya maji wakati Mbunge Ester Amos Bulaya alipofika shuleni hapo kwa ajili ya kushughulikia maboresho ya maabara.

Kwa upande wake, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Rubana, Charles Masisota, amesema tanki hilo litakuwa msaada mkubwa katika kuhakikisha maabara hiyo inapata maji ya uhakika pamoja na matumizi mengine ya shule, hasa wakati huduma ya maji inapokatika.
Amesema awali maabara hiyo mpya ilikuwa tayari imekamilika lakini haikuweza kutumika ipasavyo kutokana na kukosekana kwa mfumo wa maji ndani ya jengo hilo.

Naye Mwalimu wa Hisabati na Fizikia, Mussa Lucas Michael, amesema maboresho hayo yataongeza ufanisi wa ufundishaji kwa vitendo kwa kuwa wanafunzi wataweza kutumia vifaa vya maabara kwa urahisi zaidi.
Amesema upatikanaji wa maji, gesi na umeme utarahisisha shughuli mbalimbali za maabara ikilinganishwa na awali ambapo baadhi ya changamoto zilikuwa zikikwamisha ujifunzaji wa vitendo.
Kwa upande wao wanafunzi kupitia dada mkuu wa serikali ya wanafunzi, Juliana Jeremia, wameishukuru Ofisi ya Mbunge kwa maboresho hayo wakisema yatasaidia kupunguza changamoto zilizokuwa zikiathiri mazingira yao ya kujifunzia.