Mazingira FM
Mazingira FM
8 August 2026, 11:13 am

Baada ya tukio hilo kulifanyika operesheni ya kuwavuna mamba katika eneo hilo, huku wananchi wakihimizwa kutumia kizimba kilichopo kwa ajili ya kuoga na kuchota maji.
Na Edward Lucas
Zaidi ya miezi miwili baada ya mtoto Majura Tungaraza, maarufu Dotto, mwenye umri wa miaka saba, kuripotiwa kutoweka baada ya kushambuliwa na mamba katika Ziwa Victoria, familia yake bado haijapata mwili wala mabaki yake.
Majura aliripotiwa kutoweka Mei 21, 2026, majira ya saa 12:30 jioni, baada ya kufika kando ya Ziwa Victoria akiwa pamoja na pacha wake Kulwa na mtoto mwingine kwa ajili ya kuoga. Eneo hilo liko takribani mita 100 kutoka nyumbani kwao.
Nestina Tungaraza ambaye ni shangazi na mlezi wa watoto hao amesema tangu kupotea kwa Majura bado familia inaishi katika sintofahamu juu ya hatima ya mtoto huyo huku ikiwa na matamanio ya kupata chochote kitakachosaidia kujua hatima ya mtoto wao
Mgongo Tungaraza, mmoja wa wanafamilia, amesema tangu tukio hilo, familia imechukua hatua mbalimbali za kuwalinda watoto waliobaki, ikiwemo kuwahamisha watoto wadogo wenye umri chini ya miaka saba kutoka eneo hilo, kutokana na hofu ya kufika ziwani bila uangalizi wa wazazi au walezi.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwiseni, Musiba Kiharata, anasema baada ya tukio hilo kulifanyika operesheni ya kuwavuna mamba katika eneo hilo, huku wananchi wakihimizwa kutumia kizimba kilichopo kwa ajili ya kuoga na kuchota maji.
Hata hivyo, kijiji hicho chenye zaidi ya kaya 408 kina kizimba kimoja pekee, hali inayosababisha changamoto ya umbali na msongamano wa matumizi.
Wananchi wanasema kizimba hicho kimewasaidia kupunguza hofu wanapokwenda ziwani kwa shughuli za kufua, kuoga na kuchota maji, lakini idadi ndogo ya vizimba bado inawaweka katika mazingira magumu ya kupata huduma hizo kwa usalama.
Tukio la Majura si la kwanza katika maeneo hayo. Mwezi Mei mwaka huu, mtoto Selina Daud, mwenye umri wa miaka 17, alijeruhiwa mguu baada ya kushambuliwa na mamba akiwa ziwani akichota maji katika eneo jirani la Guta.
Wakazi wa Mwiseni sasa wanaiomba Serikali na wadau kuongeza jitihada za kuimarisha usalama wa wananchi wanaoishi pembezoni mwa Ziwa Victoria, ikiwemo kuongeza vizimba vya matumizi ya maji na kuendelea na hatua za kudhibiti mamba katika maeneo hatarishi.