Mazingira FM

Madiwani Bunda DC walia na ubovu wa barabara

15 May 2026, 11:49 pm

Baadhi ya madiwani halmashauri ya wilaya ya Bunda katika kikao cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 22025/2026

Licha ya TARURA kufanya kazi kubwa ya ujenzi wa barabara katika wilaya hiyo, baadhi ya barabara zimeharibika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni, hali inayohitaji hatua za haraka za matengenezo ili kurejesha huduma ya usafiri kwa wananchi.

Na Mariam Mramba

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda wameiomba Ofisi ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kuharakisha ukarabati wa barabara zilizoharibika katika maeneo mbalimbali ya halmashauri hiyo, wakisema hali hiyo inakwamisha shughuli za usafirishaji na kusababisha ajali kwenye baadhi ya maeneo.

Wakichangia katika kikao cha baraza la madiwani la robo ya tatu ya mwaka 2025 na 2026 madiwani hao wamesema kuwa licha ya TARURA kufanya kazi kubwa ya ujenzi wa barabara katika wilaya hiyo, baadhi ya barabara zimeharibika kutokana na mvua kubwa zilizonyesha hivi karibuni, hali inayohitaji hatua za haraka za matengenezo ili kurejesha huduma ya usafiri kwa wananchi.

Mbali na suala la barabara, madiwani hao pia wamemuomba Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuhakikisha visima vyote vilivyoharibika vinarekebishwa kwa wakati.

Aidha, wamemtaka kuhakikisha miradi yote ya maji inayotekelezwa ndani ya halmashauri hiyo inakamilika kwa wakati ili kusaidia kutatua changamoto ya upatikanaji wa maji inayowakabili wananchi katika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Sauti za madiwani Bunda DC

Akijibu hoja hizo, Meneja wa RUWASA wilaya ya Bunda malando masheku  amesema ofisi yake inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati ili wananchi waweze kunufaika na huduma ya maji safi na salama.

Sauti ya Meneja wa RUWASA wilaya ya Bunda malando masheku

Akifunga kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda amewahimiza madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo kuendelea kuwa na ushirikiano wa karibu ili kwa pamoja waweze kufanikisha maendeleo ya halmashauri hiyo.