Mazingira FM
Mazingira FM
12 June 2026, 4:15 pm

Wazee wamesema kumekuwa na ongezeko la vitendo vya kutelekezwa kwa wazazi wenye umri mkubwa, hali inayowafanya kukosa huduma muhimu ikiwemo chakula, matibabu na makazi bora.
Na Adelinus Banenwa
Wazee wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara wameiomba Serikali kutunga sheria itakayowalazimisha watoto kuwahudumia na kuwapatia matunzo wazazi wao wanapozeeka, wakidai kuwa wengi wao wamekuwa wakitelekezwa na watoto wao licha ya kuwalea na kuwapatia mahitaji muhimu wakiwa wadogo.
Ombi hilo limetolewa katika kongamano la Baraza la Ushauri la Wilaya ya Bunda lililokutana kujadili changamoto mbalimbali zinazowakabili wazee kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee, ambayo huadhimishwa kila mwaka Juni 15.

Wakizungumza katika kongamano hilo, wazee hao walisema kumekuwa na ongezeko la vitendo vya kutelekezwa kwa wazazi wenye umri mkubwa, hali inayowafanya kukosa huduma muhimu ikiwemo chakula, matibabu na makazi bora.
Mbali na kutelekezwa, wazee hao walieleza kuwa baadhi ya watoto wao huwaletea wajukuu kwa ajili ya kulelewa na baadaye kuwaacha bila kuwapatia msaada wowote wa mahitaji ya msingi, jambo linaloongeza mzigo wa maisha kwa wazee hao ambao wengi wao hawana kipato cha uhakika.

Walisema licha ya mchango mkubwa walioutoa katika malezi ya watoto wao na maendeleo ya jamii, baadhi ya watoto wamekuwa wakiwatenga na kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuwahudumia wanapofikia uzee.
Aidha, washiriki walibainisha kuwa elimu kwa jamii kuhusu haki za wazee inapaswa kuimarishwa sambamba na hatua za kisheria ili kupunguza vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya kundi hilo.
Kongamano hilo limefanyika ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Kupinga Ukatili Dhidi ya Wazee yatakayofanyika Juni 15, huku washiriki wakitoa wito kwa jamii kuendelea kuwaheshimu, kuwalinda na kuwatunza wazee kama hazina muhimu ya taifa.