Mazingira FM
Mazingira FM
22 April 2026, 8:08 pm

Watuhumiwa 14 wameachiwa huru huku wengine saba wakipatikana na kesi ya kujibu, kufuatia uamuzi mdogo (ruling) uliotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Bunda.
Na Thomas Masalu
Watuhumiwa 14 wameachiwa huru huku wengine saba wakipatikana na kesi ya kujibu, kufuatia uamuzi mdogo (ruling) uliotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Bunda chini ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mulokozi Kamuntu.
Kesi hiyo namba 21 ya mwaka 2026 ilikuwa inawakabili jumla ya watuhumiwa 21, akiwemo Katibu Mkuu mstaafu wa BAVICHA Taifa, Yohana Kaunya, pamoja na wenzake 20.
Katika uamuzi huo, mahakama imewaachia huru washtakiwa 14 baada ya kubaini kuwa mashitaka kadhaa yaliyokuwa yanawakabili, yakiwemo ya kufanya maandamano, unyang’anyi wa kutumia silaha pamoja na baadhi ya makosa ya uchomaji moto, hayakuwa na ushahidi wa kutosha.
Hata hivyo, washtakiwa saba, akiwemo Yohana Kaunya, wamepatikana na kesi ya kujibu katika baadhi ya mashitaka yaliyosalia, yakiwemo uchomaji moto, kujeruhi na kuharibu mali, baada ya mahakama kuridhika kuwa kuna ushahidi unaowahusisha.
Baada ya uamuzi huo, mahakama imeruhusu dhamana kwa masharti kwamba kila mshtakiwa atapaswa kuweka dhamana ya shilingi milioni nne au hati ya mali yenye thamani hiyo, kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya NIDA, pamoja na kutotoka nje ya Mkoa wa Mara bila ruhusa ya mahakama.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 23, 2026, ambapo washtakiwa wanaokabiliwa na mashitaka yaliyosalia wanatarajiwa kuanza kujitetea.
Akizungumza nje ya viunga vya mahakama, Wakili Gaston Garubindi, ambaye ni mmoja wa jopo la mawakili wa utetezi, alielezea kile kilichojiri wakati wa uamuzi huo.
Kwa upande wao baadhi ya vijana waliachiwa huru katika kesi hiyo wameswashukuru mawakili waliokuwa wakiwatetea katika kesi hiyo.