Mazingira FM
Mazingira FM
15 May 2026, 11:24 pm

Utoaji wa fedha hizo ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano kati ya taasisi ya Mabotto na sekta ya afya kwa lengo la kusaidia makundi yenye uhitaji maalum, hususan watoto wanaozaliwa kabla ya wakati pamoja na wananchi wenye changamoto za kiafya.
Na Adelinus Banenwa
Mkurugenzi wa Mabotto Microfinance, Robert Chacha Maboto, amechangia fedha taslimu kiasi cha shilingi laki sita kwa Hospitali ya Bunda DDH katika maadhimisho ya Siku ya Wakunga na Wauguzi yaliyofanyika Mei 15, 2026 katika viwanja vya hospitali hiyo.
Fedha hizo zinatarajiwa kusaidia kuboresha huduma za watoto wanaozaliwa kabla ya kutimiza miezi tisa pamoja na huduma nyingine muhimu zinazotolewa hospitalini hapo. Mbali na fedha hizo, mkurugenzi huyo pia ametoa mikebe 10 ya maziwa kwa ajili ya watoto hao wanaohitaji uangalizi maalum.

Akizungumza kwa niaba ya taasisi ya Mabotto, Emmanuel Kija amesema taasisi hiyo inatambua mchango mkubwa unaotolewa na hospitali hiyo kwa wananchi wa Wilaya ya Bunda na maeneo jirani. Amesema wakati Robert Chacha Maboto akiwa Mbunge wa Bunda Mjini, alishirikiana kwa karibu na hospitali hiyo katika kuhakikisha wananchi, hasa wale waliokuwa katika mazingira magumu, wanapata huduma bora za matibabu.
Aidha, amesema utoaji wa fedha hizo ni sehemu ya kuendeleza ushirikiano kati ya taasisi ya Mabotto na sekta ya afya kwa lengo la kusaidia makundi yenye uhitaji maalum, hususan watoto wanaozaliwa kabla ya wakati pamoja na wananchi wenye changamoto za kiafya.

Awali akisoma risala mbele ya mgeni rasmi katibu wa hospitali hiyo Adelad Mchuruza amesema mbali na mafanikio wanayoyapata hospiali hiyo bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo, upungufu wa vifaa tiba kama vile inkubeta ili kusaidia Watoto wanaozaliwa chini ya miezi tisa , mfumo wa oxgen hospitalini hapo miongoni mwa changamoto zingine.